Laizer aibuka na jiwe la bil. 4.86/-

04Aug 2020
Cynthia Mwilolezi
Simanjiro
Nipashe
Laizer aibuka na jiwe la bil. 4.86/-

NI Laizer tena! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Bilionea Saninniu Laizer kupata tena jiwe lingine la tanzanite lenye uzito wa kilogramu 6.33 ambalo serikali imelinunua kwa Sh. bilioni 4.86.

Bilionea Saniniu Laizer (mwenye vazi kimasai), akiwa ameshika mfano wa hundi ya zaidi ya Sh. bilioni 4.8 baada ya kuiuzia serikali jiwe la tatu la madini ya Tanzanite lenye kilo 6.33 na kukabidhiwa fedha hizo na Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kushoto), huko Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara jana. PICHA: CYNTHIA MWILOLEZI

Juni 23, mwaka huu, Laizer alipata mawe makubwa mawili yenye thamani ya Sh. bilioni 7.8, ambayo aliyauza kwa serikali na kisha kupelekwa kuhifadhiwa kwenye Makumbusho ya Taifa.

Jana, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, akizungumza katika eneo la Mirerani yaliko machimbo ya tanzanite wakati Laizer akikabidhiwa hundi ya Sh. bilioni 4.86, alisema jiwe hilo pia litahifadhiwa kwa ajili ya kuanzisha utalii wa madini.

“Tunawapenda Watanzania wanaochimba kwa haki na hawatadhulumiwa, na kila atakayepata jiwe lake atapata stahiki yake.

Serikali tunataka tuanzishe utalii wa madini nchini, na ndiyo maana leo tumenunua jiwe hili lililopatikana Juni 29 mwaka huu na tulipata taarifa siku hiyo hiyo.

“Lengo letu kubwa ni kuongeza thamani ya madini hayo nchini na kuachana na kunufaisha nchi zingine kwa malighafi," Bitoke alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kupitia unuzuzi huo, serikali imepata mrabaha wa Sh. milioni 293, jambo ambalo linaipa nguvu ya kuongeza maeneo ya uthaminishaji madini.

Aliwataka Watanzania na wachimbaji kupuuza wanaolidanganya taifa kuwa serikali inamdhulumu Bilionea Laizer, kwa kuwa kabla ya ununuzi huo, wametumia wathaminishaji watatu kufanya tathmini ili kumlipa stahiki yake.

Kuhusu wanaoendelea kutorosha madini kwenda nje ya nchi, Biteko alionya kuwa hakuna mfanyabiashara atakayetoboa au kufanikiwa kutekeleza dhamira hiyo.

"Vyema mkajua pale mnapokuwa watatu au wawili, mkapanga njama zenu mjue mmoja wenu atatupa taarifa zenu zote. Na mnapopumua, mjue na sisi serikali tunafahamu mbinu zenu mpya zote mlizobuni.

"Serikali ina fedha nyingi na itaendelea kununua madini yenye uzito mkubwa ili dunia ije Tanzania kutalii na kuongeza mapato yetu.

"Katika hili, kila siku ninapata simu za nje ya nchi, wakiomba kununua mawe haya tulionunua kwa Bilionea Laizer na mimi ninawajibu kwa kiburi 'tuna fedha tunanunua wenyewe', maana tumechoka kuzalisha malighafi za nchi zingine," alisema.

Waziri huyo pia aliwataka wachimbaji wadogo kuendelea kusubiri utaratibu unaowekwa na serikali kuhusu uchimbaji kwenye Kitalu C ambacho ubia kati ya serikali na mwekezaji umevunjika.

Waziri Biteko alionya uvamizi huo akisema: "Msivamie pale panalindwa, na atakayeingia hapo hakuna atakayemsaidia. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu hatuna mpango wa kuwapa wawekezaji tena, maana kwa miaka mingi walipokuwapo hatujawahi pata jiwe la uzito wa kilogramu tisa, saba, wala tatu.

“Ni bora tuendelee kuwaongezea ujuzi wachimbaji wadogo, ambao sasa wameonyesha maajabu na Tanzania kuongoza duniani, kwa kuwa na mawe yenye uzito mkubwa."

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, aliwataka wananchi kuwa wazalendo, ili madini hayo yanufaishe wote na ili kulinda rasilimali hizo vema kila mmoja akatumia haki yake ya kupiga kura kwa kuchagua viongozi watakaoendeleza sekta hiyo na kupageuza Mirerani kuwa sehemu ya maajabu.

Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kulinda rasilimali za nchi ili kila mmoja anufaike nazo.

Bilionea Laizer alishukuru serikali kwa kununua madini hayo na kuwaomba wachimbaji wenzake kuendelea kuwa wazalendo, ili kuinua uchumi wa taifa.

"Wale wanaosema nimedanganywa, hapana wala sijadanganywa wala kuibiwa, ni waongo. Serikali imenipa stahiki yangu na kweli serikali hii haina mfano kwani imewaleta maendeleo makubwa yakiwamo maji kwenye vijiji vya umasaini ambako walikuwa wakitumia punda kutafuta maji umbali mrefu, sasa tumeachana nao," alisema.

Habari Kubwa