Latra kupanga bei elekezi usafiri wa teksi

12Jun 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Latra kupanga bei elekezi usafiri wa teksi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Barabara Ardhini (Latra), imesema iko katika hatua za mwisho za kuandaa kanuni za bei elekezi ya usafiri wa teksi nchini.

teksi.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Latra, Johansen Kahatano, alisema kanuni hizo zimeshakamilika zinasubiri kupelekwa kwa wadau kwa ajili ya maoni.

Alisema kanuni hizo zitakamilika kabla ya Julai mwaka huu na kuanza kutumika kabla ya mwaka wa fedha.

"Nyaraka iko tayari kinachofuata ni kuipeleka kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni, wadau wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kabla ya kusainiwa na kuanza kazi," alisema.

Kwa mujibu wa Kahatano, wamefikia uamuzi wa kuwa na kanuni hizo kutokana na usafiri huo kutokuwa na bei elekezi bali kila mtu kutoza fedha kwa kufikiria na maamuzi ya dereva mwenyewe.

"Malalamiko ya wadau wa usafiri wa teksi yalikuwa mengi sana na serikali inakosa mapato kwenye eneo hilo, tunakuja na kanuni za kusimamia kwa kuwa tumeona ni muhimu kusimamia," alisema.

Kwa mujibu wa Kahatano, ni lazima watumiaji wa magari hayo wajue nauli za maeneo mbalimbali na siyo kukadiria kwa kumwangalia abiria usoni.

Alisema pia katika makadirio hayo serikali inapoteza fedha na kuwa na utaratibu wa bei elekezi itasaidia kuweka usawa, na kwamba lilikuwa hitaji la watumiaji na wenye teksi.

Habari Kubwa