LATRA, Vodacom zashirikiana kukata tiketi kimtandao

05Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
LATRA, Vodacom zashirikiana kukata tiketi kimtandao

KAMPIUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji Nchi Kavu (LATRA) kuzindua huduma ya mtandao itakayowezesha abiria kuweka nafasi na kununua tiketi za mabasi kupitia huduma ya M-Pesa.

Huduma hiyo kwa sasa inapatikana kwenye ofisi za waendeshaji wa kampuni tatu za mabasi, ambazo ni Majinjah Logistics Limited, Tungi Express na Maning Nice, ambayo yanafanya safari zake karibu nchi nzima.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi, alisema wateja wanaweza kupata huduma kwa kupakua zana (App) ambayo inapokea malipo kwa kupitia M-Pesa.

“Kwa kupitia zana (App) hii wateja wanaweza kuchagua kampuni ya mabasi, tarehe anayopenda kusafiri, muda na kuchagua namba ya siti," alisema Hendi.

Alisema Vodacom kama kampuni ya teknolojia na mawasiliano inasaidia wateja wake kukamilisha mambo mengi wakiwa mbali na watoa huduma.

“Na huu ni uvumbuzi mpya kuonyesha jinsi ambavyo teknolojia inaweza kusaidia kuongeza utamaduni wa kupata huduma ukiwa mbali na mtoa huduma, jambo ambalo hatimaye linajenga jamii ya kidigitali,” alisema Hendi.

Alifafanua kwamba mteja anaweza kupokea tiketi yake halisi atakapofika katika ofisi ya basi au kituoni wakati wa safari, hii ni baada ya kuonyesha ujumbe mfupi aliotumiwa baada ya kuthibitisha malipo yake aliyotuma kwa njia ya M-Pesa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe, aliunga mkono juhudi hizo na kusema kwamba huduma hii imekuja katika wakati muafaka kusaidia serikali katika ukusanyaji wa kodi.

“Malipo yataenda moja kwa moja serikalini kupitia National Internet Data Center (NIDC) jambo ambalo litasaidia kuwapo kwa uwazi wa makusanyo yote na hivyo serikali kupata kodi stahiki na kwa wakati," alisema Ngewe.

Alisema mikakati ya kuongeza idadi ya watoa huduma inaendelea na hivi karibuni kampuni zote za usafiri kwa njia ya mabasi watakuwamo katika zana (App) hii ili kuwarahisishia abiria ukataji wa tiketi.

Habari Kubwa