Latra yafungua milango usafiri daladala

03Apr 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Latra yafungua milango usafiri daladala

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), imewataka watu binafsi, shule na taasisi zenye mabasi ambayo hayajapangiwa njia kwa ajili ya usafirishaji, kuomba leseni za muda mfupi kwa ajili ya kutoa huduma hiyo katika maeneo ya mijini.

Latra katika taarifa yake kwa umma jana, imeamua kufanya hivyo kwa sababu ya ongezeko la uhitaji wa vyombo vya usafiri wa abiria kutokana na utekekelezaji wa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.

“Latra inawataarifu wadau wa usafiri wa umma nchini kuwa kufuatia (kutokana na) utekelezaji wa tahadhari dhidi ya corona, kuna ongezeko la uhitaji wa vyombo vya usafiri wa abiria,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa wadau watakaoitikia wito huo, watapaswa kufika katika ofisi za Latra zilizo karibu yao wakiwa na kadi za magari.

Taarifa hiyo ya Latra imekuja ikiwa siku moja tu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutoa kibali cha usafiri wa pikipiki za miguu mitatu (bajaji) na bodaboda kusafirisha abiria katikati ya jiji hilo.

Alisema lengo la kutoa kibali hicho ni kusaidia kusafirisha abiria ambao watakuwa na uwezo wa kutumia usafiri huo kuwahishwa kazini na kupunguza changamoto iliyopo kwa sasa usafiri inayosababishwa na hatua zinazochukuliwa juu ya tahadhari ya ugonjwa wa corona.

Jumatatu ya wiki hii, agizo la magari za umma kubeba abiria kulingana na idadi ya viti vyake, lilianza kutekelezwa rasmi, hivyo kuongeza changamoto ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Katika vituo vingi vya mabasi vikiwamo vya mwendokasi, foleni ya watu katika dirisha za kukatia tiketi hadi mchakato wa kusafiri kwenda katika maeneo mbalimbali imekuwa kubwa.

Sambamba na hilo, kumekuwa na watu wengi vituoni huku baadhi ya daladala zikiwalazimisha watu kukaa chini na baadhi yao kutumia zaidi za saa tano kuhangaikia usafiri.

Habari Kubwa