Lema ajitosa kugombea tena ubunge Arusha

09Jul 2020
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Lema ajitosa kugombea tena ubunge Arusha

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Godbless Lema, leo amechukuwa fomu ya kugombea nafasi ya ubunge  wa jimbo hilo, kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika  Oktoba mwaka huu.

Mke wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini , Godbless Lema, Neema Lema, akikabidhiwa fomu ya Lema kugombea tena nafasi ya ubunge wa Arusha Mjini leo kupitia Chadema na Katibu wa Chadema, Jimbo la Arusha Mjini, Mosses Nanyaro. Picha : Allan lsack

Lema ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, alikuwa  Mbunge  wa Arusha Mjini kwa kipindi cha miaka 10.

Akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya Lema, wakati wa hafla fupi ya uchukuaji wa  fomu, kwenye Ofisi za Chadema, Kanda ya Kaskazini, Mke wa Lema, Neema Godbless Lema, amesema aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, alishindwa kuhudhuria hafla ya uchukuaji wa fomu kwa kuwa alikuwa kwenye majukumu mengine ya kichama. 

"Lema ameshindwa kufika hapa ofisi za chama kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge jimbo la Arusha Mjini, hivyo ameniomba mimi kumuwakilisha kuchukua fomu kwa niaba yake,"amesema Neema. Katibu wa Chadema Arusha Mjini, Mosses Nanyaro, amesema kwa sasa chama hicho, kipo katika hatua ya wagombea wa nafasi ya uraisi,ubunge na udiwani kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Amesema zoezi la kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama kuwateua kugombea nafasi mbalimbali za uongozi lilianza Julai 4 mwaka huu na zoezi hilo litafungwa Julai 10.

Hata hivyo, amesema kwa mujibu wa utaratibu wa Chadema unaruhusu wakala kumchukulia fomu mgombea na baada ya kukamilisha utaratibu fomu hizo zinarudishwa kwenye chama. 

Licha ya kuzungumza hayo, amesema Chadema wamejipanga kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. 

"Hujuma zilitofanyika kwenye Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana hatutarajii zitatokea mwaka kwa kuwa tumejipanga kushinda uchaguzi," amesema Nanyaro. 

Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe, amesema wanachama wa Chadema waliyohama  chadema na kujiunga na CCM, wanapaswa  kutambua kuwa chama hicho, kina utaratibu wa kufanya tathimini ya utendaji kazi wa viongozi wake, baada ya kumaliza muda wao, hivyo wengi wao waliohama chama wasingepewa nafasi kwenye chama. 

Akizungumzia kuhama kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, na kujiunga na CCM, kiongozi huyo, wa Chadema, amesema Julai 4 mwaka huu, Nassari alimtumia ujumbe mfupi kuhusu kuhakikishiwa na chama kupewa ridhaa ya kugombea tena ubunge mwaka huu.

"Nassari aliomba kuhakikishiwa na chama nafasi ya kugombea tena ubunge lakini tulimueleza utaratibu wa chama lazima ufuatwe na kuzingatia, amesema.

Habari Kubwa