Lema ngoma bado nzito

29Nov 2016
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Lema ngoma bado nzito

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), jana alikwama tena kutoka mahabusu ambako amekaa kwa wiki nne ama Kituo Kikuu cha Polisi Arusha au Gereza la Kisongo, baada ya Jamhuri kupinga usikilizaji wa rufani yake.

Lema alikata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wiki iliyopita akipinga kunyimwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha pingamizi mahakamani hapo ukiomba asipewe dhamana katika kesi yake ya uchochezi.

Pingamizi la jana katika Mahakama Kuu lilisababisha wafuasi wa Lema waliofika Mahakamani hapo saa moja asubuhi baadhi wakiwa wamevaa fulana zenye picha ya Lema na mgongoni kuandika maneno ya “Justice (Haki) 4 (Kwa) Lema”, kuangua kilio.

Jaji Fatuma Masengi aliyekuwa amepanga kutoa maamuzi ya rufani ya Mbunge huyo katika moja ya vyumba vya mahakama hiyo, alilazimika kuahirisha usikilizaji huo ofisini kwake, kufuatia pingamizi hilo.

Akizungumza eneo la Mahakama Kuu baada ya kutoka kwa jaji Masengi, wakili wa Serikali Martenus Marandu akisaidiana na Paul Kadushi alisema wamewasilisha pingamizi la kupinga rufani hiyo.

Alisema wamepinga kusikilizwa kwa sababu upande wa Lema umewasilisha rufani hiyo Mahakama Kuu bila kutoa kusudio la kukata rufani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Alisema kutokana na pingamizi hilo, Jaji Fatuma Masengi amewataka awasilishe hoja za pingamizi lao kesho saa mbili asubuhi kimaandishi na ifikapo saa sita mchana, mawakili wa Lema wajibu kimaandishi.

Aidha walisema baada ya Jaji kupokea hoja za pande zote mbili, atatoa uamuzi wa pingamizi hizo Ijumaa, wa ama kulitupa pingamizi hilo au kusikiliza rufani ya Lema ya kutaka haki ya dhamana.

Lema alitolewa chumba cha mahabusu saa 7:08 mchana na kuingizwa kwenye basi la Magereza huku wafuasi wake wakilia.

IPO WAZI
Wiki mbili zilizopita, mawakili wa Lema walisema wameamua kufungua maombi ya rufani ili waelezwe sababu za mteja wao kukosa dhamana ambayo awali Hakimu Desdery Kamugisha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha alisema ipo wazi.

Walisema sababu ya kufungua rufani ambazo ni kutokana na kutoridhishwa na hatua ya Hakimu Kamugisha kumnyima dhamana Lema, huku akijua kuwa alifanya kosa kwa kuwa tu mawakili wa serikali wakiongozwa na Kadushi walisema wameonyesha nia ya kukata rufani.

Awali katika hoja za mawakili wa serikali wakiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi, Kadushi, walipinga Lema kupewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa madai kuwa amefanya kosa aliloshtakiwa nalo akiwa amepewa dhamana na mahakama hiyo katika shtaka lingine kama hilo.

Pia walidai kuwa Lema kupewa dhamana kulikuwa na hatari ya usalama wa maisha yake.

Akitupilia mbali hoja hizo, Hakimu Kamugisha alisema mahakama haitoi dhamana kama hisani, bali ni haki ya msingi ya mtuhumiwa kama ilivyoainishwa katika Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.

Alisema iwapo mtuhumiwa ananyimwa dhamana, sheria inatakiwa kutamka bayana.

Habari Kubwa