Lema sasa apewa siku 10 ajinasue

21Dec 2016
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Lema sasa apewa siku 10 ajinasue

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha imekubali ombi la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuongezwa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukatia rufani pingamizi la kupewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha huku ikimpa siku 10 kujinasua.

Akitoa uamuzi wake jana kuanzia saa 6:26 hadi majira ya saa saba mchana, Jaji wa Mahakama Kuu, Dk. Modesta Opiyo, alisema mahakama hiyo imeruhusu maombi ya kuwasilisha notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufani kupinga kunyimwa dhamana.

Jaji Opiyo alisema hoja za upande wa Serikali zilizowasilishwa na Wakili Hashim Ngole za kudai waleta maombi hayo walikuwa wazembe na walichelewa siku nne kuwasilisha notisi baada ya rufani yao kuondolewa na Jaji Fatuma Masengi Desemba 2, mwaka huu hazina mashiko.

Alisema kuondoa kesi mahakamani haimaanishi kuwanyima fursa ya kupigania nia ya kukata rufani, kwa kuwa milango ilikuwa wazi.

Aidha, Jaji Opiyo alisema hoja ya siku nne zinazolalamikiwa kuwa walichelewa kutoa maombi hayo, hazina mashiko kwa kuwa siku mbili kati yake (Jumamosi na Jumapili) zilikuwa za mapumziko, hivyo walitumia siku mbili kuandaa nyaraka na kuwasilisha maombi hayo mahakamani.

Alisema katika maombi hayo, wametoa pia sababu za nia ya kutaka kukata rufani na sababu hizo ziko wazi.

“Katika hili, hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa. Mahakama hii inatumia busara zake kuruhusu maombi haya ya kutoa notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufani juu ya dhamana yake Mbunge huyu,” alisema.

Jaji Opiyo alisema Mahakama Kuu inatoa siku 10 kuanzia uamuzi huo utolewa mleta maombi (Lema) kuwasilisha notisi yake ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufani.

Aidha, kuhusu hoja ya mawakili wa Lema ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa uvunjifu wa sheria uliofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha juu ya kuruhusu dhamana na baadaye mikono yake kufungwa na kushindwa kutoa masharti ya dhamana, baada ya Mawakili wa Serikali kuonyesha nia ya kukata rufani, Jaji Opiyo alisema mahakama hiyo haiwezi kuzungumzia hilo kwa sasa.

“Wakati mwafaka wa kuzungumzia suala hilo la kuhusu dhamana ni pale rufani ya dhamana itakapokatwa, ila leo (jana) ilikuwa tu kutoa uamuzi juu ya kuruhusu au kukataa maombi ya kuongezewa muda wa notisi na ndio tumetoa na asiyeridhika ruksa, kukata rufani,” alisema.

Pingamizi za mawakili wa Serikali zilitupwa Desemba 16, mwaka huu na Jaji Opiyo, baada ya kupitia hoja za pande zote na kusema kuwa mawakili hao hawakuwa na hoja za kisheria zenye mashiko.

Katika maombi hayo namba 69, upande wa Serikali ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.

Awali akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufani hiyo isikilizwe, Wakili Mfinanga alidai mahakamani hapo kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufani ni uliotolewa Novemba 11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambao Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Uamuzi huo unamfanya Lema aruke kihunzi cha pili baada ya kutupwa kwa pingamizi za Serikali na kusikiliza maombi hayo na pia Mahakama Kuu kumkubalia ombi la kuongezewa muda akate rufani.

Wakili Mfinanga aliiambia Nipashe jana mchana kuwa tayari ameshatoa notisi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na
kupokewa.

Ilipofika saa 12:20 jioni, Wakili Mfinanga aliliambia gazeti hili kuwa walifanikiwa kusajili rufani na kupewa namba 126 ya mwaka 2016 na wanasubiri kupangiwa Jaji.

Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anashikiliwa na vyombo vya dola kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa akiwa mahabusu kwenye Gereza Kuu la Kisongo.

Alikamatwa Novemba 2, mwaka huu kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusafirishwa usiku kuja jijini hapa kabla ya kufikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Magufuli.

Habari Kubwa