Leseni  za vituo  luninga kupitiwa

06Dec 2017
Mary Geofrey
Nipashe
Leseni  za vituo  luninga kupitiwa

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema inafanya mapitio ya leseni za vituo vya luninga ili kufanyia utatuzi kasoro zilizojitokeza wakati wa kuhama kutoka mfumo wa analojia kuelekea digitali.

 

Aidha, imezitaka kampuni zinazorusha matangazo ya luninga kufuata sheria na kanuni za usajili zinazowataka kurusha bure matangazo ya chaneli za ndani.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, aliyaeleza hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alipofanya ziara katika ofisi hizo.

Kilaba alisema kuhama kutoka analojia kwenda digitali ilikuwa ni kazi kubwa ambayo lazima ingeleta changamoto ambazo wanaendelea kuzifanyia kazi.

Alisema kampuni hizo zimekuwa zikikata matangazo ya chaneli za ndani pindi muda wa kifurushi alicholipia mteja kumalizika licha ya mkataba walioingia na TCRA kuelekeza kuwa huduma hizo zitatolewa bure kwa wananchi.

Alisema anatambua kuwapo mvutano kati ya kampuni za urushaji matangazo na watoa huduma wa kituo kuwa nani anapaswa kulipia gharama hizo na ni kiasi gani na kwamba wanalitafutia ufumbuzi suala hilo ili wananchi wapate chaneli hizo bure.

Chaneli zinazotakiwa kupatikana bure ni ITV, TBC, Star TV, Chanel Ten, Clouds TV na TV Tumaini.Naye Naibu Waziri huyo, aliwataka TCRA kusimamia kanuni na sheria hizo ili wananchi wapate huduma hizo bila malipo yoyote.

Aidha, Nditiye, aliitaka TCRA kufunga vibanda vyote vya kusajili laini za simu bila kufuata sheria.Alisema kumekuwapo na idadi ya vibanda na watu wakipita mitaani bila kuwa na vitambulisho na kusajili laini bila kuzingatia kanuni na taratibu za usajili hali ambayo inapelekea baadhi yao kuzitumia kufanya uhalifu.

“Tunataka kila mtu anayetumia laini awe anafahamika. Na taratibu zitumike kama ilivyopangwa kuwa vitambulisho vinavyotakiwa kutumika ni vya kupigia kura au cha uraia. Napendekeza ikiwezekana usajili uwe unafanyika kwenye ofisi za watoa huduma badala ya watu kusajili ovyo mitaani,” alisema. 

  

Habari Kubwa