LHRC watia neno kijana aliyefungwa minyororo

13Nov 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
LHRC watia neno kijana aliyefungwa minyororo

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amelaani tukio lililofanywa dhidi ya Shadrack Johanes (26), mkazi wa Old Shinyanga mkoani Shinyanga, kwa kufungwa minyororo chumbani miezi miwili na ndugu zake.

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, picha mtandao

Akizungumza na Nipashe jana kuhusu tukio hilo, Henga alisema kilichofanywa dhidi ya kijana huyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na katiba ya nchi.

Alisema ndugu zake walipaswa kumpeleka katika hospitali zinazotoa matibabu ya afya ya akili ili atibiwe badala ya kumfungia ndani kisa anasababisha uharibifu mitaani.

Alibainisha kuwa ibara za 12 na 13 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, zinapinga vitendo hivyo kwa mtu yeyote kubaguliwa kutokana na sababu ya ulemavu alionao.

Henga alisema ibara hizo zinaweka masharti ya kila mtu kuheshimiwa utu wake na kupewa haki zote anazostahili.

“Sisi (LHRC) tunalaani tukio hili lililofanywa dhidi ya Shadrack kwa kufungwa minyororo chumbani na ndugu zake kwa miezi miwili, huku akiwa uchi wa mnyama," alisema.

“Ukisoma ibara ya 12 ya katiba ya nchi, inasema binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, na ibara ya 13 inasema kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, na kijana huyu hakuthamiwa," alisema.

Mama Mzazi wa Shadrack, Nonja Kalala, aliyeamua kumchukua mtoto wake huyo na kumpleka jijini Mwanza kwa matibabu, alisema kwa sasa anaendelea vizuri na wamelazimika kumpatia lishe maalum ili kuimarisha afya yake iliyokuwa imedhoofika kutokana na kufungiwa chumbani kwa muda mrefu.

"Nalishukuru gazeti la Nipashe kwa kumwibua kijana wangu, mimi ninaishi Mwanza, mwanangu alikuwa akiishi Shinyanga na shaghazi yake pamoja na kaka yake, nilikuwa sijui chochote kile juu ya mwanangu kama anafanyiwa ukatili huo," alidai.

Habari Kubwa