LHRC yatoa mapendekezo manne kumaliza mkwamo kesi mashekhe

16Mar 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
LHRC yatoa mapendekezo manne kumaliza mkwamo kesi mashekhe

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu, kimetoa mapendekezo manne kwa serikali ili kumaliza mkwamo wa kesi ya mashekhe waliopo mahabusu katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.

Katibu wa Taasisi ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dar es Salaam jana, wakati akiiomba serikali kuwaachiwa huru mashekhe wote wanaotuhumiwa kwa ugaidi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk. Anna Henga. PICHA: SABATO KASIKA

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya kituo hicho, Kijitonyama Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisema kuna haja kwa serikali kumaliza kesi hiyo.

"Tunapendekeza Mwendesha Mashtaka wa Serikali awafutie mashtaka au awafikishe mahakamani kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kuzingatia haki za kikatiba," alisema Anna.

Alisema kwa wiki mbili kumekuwa na mjadala mkubwa unaoendelea katika jamii, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kifo cha Shekhe Said Mohamed Ulatule (80).

"Shekhe huyo aliripotiwa kufariki dunia Machi 4, mwaka huu akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam," alisema.

Alisema Mwendesha Mashtaka wa Serikali, katika kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kama yalivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, anaweza kumaliza mkwamo huo.

"Pendekezo letu la pili ni kwamba ufanyike uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha kifo cha Shekhe huyo na utaratibu huo uendelee kwa wote wanaopoteza maisha wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo Sura ya 24 ya mwaka 1980 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019," alisema.

Katika pendekezo la tatu, Anna anaishauri serikali kuwaachia huru au iwape haki ya kujitetea mahakamani watuhumiwa wote waliokaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja bila mashauri yao kusikilizwa.

"Katika pendekezo la nne, tunashauri Haki Jinai inayoendelea na zoezi la kukusanya maoni nchini, itumie fursa hii kupendekeza kwa Rais watuhumiwa wote wa makosa ya ugaidi waliokaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja, ambao baadhi yao wamefikisha miaka 10 bila kesi zao kusikilizwa, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), awaachie huru, hasa kwa kuwa viashiria vingi vinaonyesha uwapo wa uonevu badala ya ukweli," alisema.

Katibu wa Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, alisema watu wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini, kwa tuhuma za ugaidi na kushauri sakata hilo limalizwe.

"Mambo mengi ya maridhiano yamejikita zaidi kwenye siasa, lakini upande huu ambao leo tunaouzungumzia ni kama umesahaulika," alisema Shekhe Ponda.

Katibu huyo alifafanua kuwa lengo lao sio kuzungumzia walioko magerezani, bali mfumo mzima wa haki za binadamu ili usaidie kuishi kwa amani.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya kituo hicho jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Anna Henga, alisema Kuna haja kwa serikali kumaliza kesi hiyo.

"Tunapendekeza Mwendesha Mashtaka wa Serikali awafutie mashtaka au awafikishe mahakamani kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kuzingatia haki za kikatiba," alisema Anna.

Alisema kwa wiki mbili kumekuwa na mjadala mkubwa unaoendelea katika jamii, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kifo cha Shekhe Ulatule.

Habari Kubwa