Licha ya corona Mo Dewji azidi kung'ara orodha ya mabilionea

25Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Licha ya corona Mo Dewji azidi kung'ara orodha ya mabilionea

LICHA ya mlipuko wa virusi vya corona, mabilionea wa Afrika wameongeza utajiri wao kulinganishwa na miaka minane iliyopita, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji 'Mo', akiwa miongoni mwa mabilionea 18 barani waliopenya kwenye orodha mpya ya Jarida la Forbes.

Mohammed Dewji 'Mo'.

Kwa mujibu wa ripoti ya jarida hilo iliyotolewa jana, mabilionea hao wa Bara la Afrika wana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 84.9 ikiwa ni asilimia 15 zaidi ya miezi 12 iliyopita na ongezeko la juu zaidi tangu mwaka 2014 wakati bara lilipokuwa na mabilionea 28 waliokuwa na utajiri wa jumla ya Dola bilioni 96.5.
 
Katika utafiti wake, Forbes imeripoti kuwa ilitumia vigezo vya akiba ya mali na viwango vya kubadilisha fedha kwa  tarehe 19 Januari mwaka huu kupima thamani ya utajiri wa mabilionea hao.
 
Kwa mujibu wa Forbes, mabilionea 18 waliopenya kwenye orodha hiyo wametoka kwenye nchi saba, Afrika Kusini na Misri zikiongoza kwa kuingiza watano kila moja, zikifuatwa na Nigeria yenye mabilionea watatu.
 
Kwenye orodha hiyo, Mtanzania Mo Dewji amefungana na Othman Benjelloun (Morocco) na Yousef Mansour (Misri) katika nafasi ya 15, wote wakiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.5 kila mmoja.
 
Katika ripoti yake hiyo, Forbes imebainisha kuwa imezingatia utajiri wa mabilionea wanaoishi Afrika au ambao biashara zao zina mzizi na zinafanyika ndani ya bara hilo.
 
Kwa kuzingatia kigezo hicho, ripoti mpya ya Forbes imewaweka nje ya orodha mzaliwa wa Sudan Mo Ibrahim, aliyechukua uraia wa Uingereza na mzaliwa wa Misri Mohamed Al-Fayed anayeishi London. Hata hivyo raia wa Zimbabwe Strive Masiyiwa, anayeishi London, amepenya kwenye orodha kwa sababu ya uwekezaji wake katika masuala ya mawasiliano barani Afrika.
 
Ripoti ya Forbes imebainisha kuwa mabilionea wawili kati ya 18 wameporomoka kiutajiri kulinganishwa na mwaka uliopita. Hao ni Mo Dewji wa Tanzania na Koos Bekker wa Afrika Kusini.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utajiri wa Mo Dewji umeshuka hadi Dola bilioni 1.5 kutoka Dola bilioni 1.6 mwaka mmoja uliopita kutokana na ushindani wa kibiashara wakati Bekker akiporomoka hadi Dola bilioni 2.7 kutoka Dola bilioni 2.8 kutoka na hisa za wabia wake katika masuala ya biashara ya mawasiliano ya intaneti, Naspers na Prosus kupungua kwa zaidi ya asilimia 20 kwa kila mbia.
 
Ripoti ya Forbes imebainisha kuwa kwa miaka 11 mfululizo sasa, Aliko Dangote wa Nigeria ameendelea kuwa tajiri namba moja barani Afrika, ajiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani biliono 13.9, akipanda kutoka Dola bilioni 12.1 mwaka jana, sababu kuu ikiwa ni kuongezeka kwa asilimia 30 kwa mauzo ya saruji ya Dangote ambayo ndiyo uwekezaji wake mkubwa zaidi.
 
“Mabilionea wote barani Afrika ni wanaume; mwanamke wa kwanza kupenya kwenye orodha, Isabel dos Santos wa Angola, alianguka kwenye ripoti ya Forbes ya Januari 2021,” ripoti inahitimisha.

Habari Kubwa