Likizo corona yaibua wanafunzi 40 wajawazito

02Jul 2020
Ambrose Wantaigwa
Bunda
Nipashe
Likizo corona yaibua wanafunzi 40 wajawazito

SERIKALI wilayani Bunda, mkoani Mara imeanzisha msako wa watuhumiwa wa ubakaji na kuwapa ujauzito wanafunzi zaidi ya 40.

Hali hiyo ya wanafunzi kupata ujauzito imegundulika wakati walipoanza kuripoti shuleni kuanzia wiki hii katika hatua ya msingi na sekondari baada ya likizo ya corona.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, alisema wakati akipokea ripoti ya utekelezaji wa ilani ya serikali, kuna wasiwasi idadi hiyo ikaongezeka.

Alisema kuanzia mwezi Januari hadi Juni, mwaka huu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 26, walipata ujauzito, huku matukio mengine 19 ya ubakaji yakiripotiwa wilayani hapa.

“Serikali imeanzisha msako mkali kwa wale wote waliohusika na unyanyasaji huu kwa namna moja au nyingine wakiwamo wazazi wanaodaiwa kuwaozesha mabinti hao na kupokea mahari," alisema Bupilipili.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 80 imetekelezwa wilayani hapo ikiwamo ya elimu, afya, barabara na maji.

Kulingana na asasi za kiraia zinazotetea haki za wanawake na watoto wilayani humu, sababu zinazohusishwa na kuongezeka kwa matukio ya ukatili huo wa watoto ni pamoja na imani za kishirikina na umaskini.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kivulini, Yassin Ally, alisema asasi hiyo imefadhili masomo ya mtoto mmoja aliyedaiwa kubakwa na baba yake mzazi hadi ngazi ya chuo kikuu.

Habari Kubwa