Lipumba aishauri serikali kukopa BoT

24Jun 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Lipumba aishauri serikali kukopa BoT

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, ameishauri serikali kukopa fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa lengo la kuongeza ujazi wa fedha kwenye mzunguko wa fedha nchini, ili kutatua changamoto ya hali ngumu ya kibiashara kwa wananchi.

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba.

Akizungumza juzi kwenye kongamano la Haki na Furaha kwa Wote katika uzinduzi wa sera ya furaha kwa wananchi wote, Prof. Lipumba alisema hali ngumu ya kibiashara wanayokutana nayo wafanyabiashara wengi nchini inatokana na kupungua kwa ujazi wa fedha katika mzunguko wa fedha nchini.

“Moja ya tatizo ni kwamba mzunguko wa fedha katika uchumi umepungua, ujazi wa fedha mwaka 2015 ulikuwa kwa asilimia 14.5, mwaka 2016 ukuaji wa ujazi wa fedha ukapungua chini ya asilimia moja, mwaka 2017 ukawa kama asilimia 1.3, mwaka 2018 ukawa chini ya asilimia moja kwa wastani wa miaka mitatu iliyopita,” alisema na kuongeza:

“Ujazi wa fedha za msingi ukuaji wake upo chini ya asilimia moja wakati hatuna tatizo la mfumuko wa bei.”

Kwa mujibu wa Prof. Lipumba, miaka mitatu ya mwisho ya uongozi wa awamu iliyopita, ujazi wa fedha ulikuwa kwa asilimia 15 na kwamba kwa sasa umeporomoka na kufikia chiniya asilimia moja.

“Wananchi wanalalamika kwamba vyuma vimekaza, lakini ukitazama takwimu hali ni nzuri, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alikuwa mzee wa kutumia ujazi wa fedha wakati wake ulikuwa unaongezeka kwa asilimia 15 kipindi cha miaka mitatu iliyopita umeporomoka chini ya asilimia moja, lazima patakuwa na tatizo katika mzunguko wa fedha,” alisema Lipumba ambaye ni profesa wa uchumi.

Prof. Lipumba pia alishauri serikali kuwekeza katika sekta ya kilimo, akieleza kuwa kilimo ndio tegemeo la wananchi wengi na kuwa bila kuwekeza katika kilimo ni vigumu kupiga hatua katika sekta ya viwanda.

“Nimekuwa napitia kitabu cha hali ya uchumi wa taifa kuna jedwali humu la 24 ukilifanyia kazi unakuta mwaka wa fedha 2017/2018 huwezi ukaamini kwenye kila Sh. 100 iliyotumiwa na serikali fedha iliyokwenda kwenye sekta ya kilimo ni Sh. 1, huwezi ukaamini mpaka nikadhani labda walikosea nikafanya hesabu napata hiyo hiyo asilimia moja,” alisema.

JIBU LA BoT

Gazeti lilimtafuta Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga, ili kutoa ufafanuzi wa hoja ya Prof. Lipumba, alitaka atafutwe Meneja msaidizi wa Benki hiyo ili atoe ufafanuzi na alipotafutwa Meneja Msaidizi, Zalia Mbeo, akisema hoja hiyo inaihusu serikali na kuwa ndio inayoweza kutoa ufafanuzi wa suala hilo.

“Kwa kuwa ameishauri serikali basi ungeitafuta serikali ndio inaweza kuwa na majibu mazuri,” Zalia alisema.

UCHAGUZI WA MWAKANIKuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2020, Prof. Lipumba alisema chama hicho kitaendelea kudai demokrasia ya kweli na kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yatakuwa sehemu ya sera na pia ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

“Kama kuna demokrasia ya kweli uko salama wakati unatoka madarakani, lakini pakiwa hakuna demokrasia ya kweli, mambo yanaweza kugeuza kibao, uliyokuwa unayafanya mazuri ya kutetea rasilimali ili zitumiwe kwa manufaa ya Watanzania mambo hayo yakageuzwa,” alisema.

WAPOKEA CHADEMA, ACT

Katika mkutano huo pia chama hicho kilipokea wanachama kutoka vyama viwili vya upinzani wengi wao kutoka Chama cha ACT-Wazalendo na wengine kutoka Chama cha Demokrasia naMaendeleo (Chadema).

Habari Kubwa