Lipumba aahidi uchumi wa korosho, gesi kusini

20Oct 2020
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Lipumba aahidi uchumi wa korosho, gesi kusini

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Wananchi ( CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, amesema akichaguliwa, atahakikisha serikali yake inaongeza thamani ya zao la korosho kwa mikoa ya kusini.

Amesema ataanzisha  viwanda vya kusindika mazao na kutengeneza juisi ya mabibo yanayotokana na korosho.

Lipumba aliyasema hayo wilayani Masasi mkoani Mtwara alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa wilaya hiyo kwenye mkutano wake wa kampeni.

Alisema  mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo kama zikitumika vizuri uchumi wa mikoa hiyo utapanda na kupunguza umasiki unayowakabili wakazi wa mikao hiyo.

Lipumba alisema kuwa iwapo akichaguliwa kuwa rais atahakikisha anaanzisha viwanda vya kutosha vikiwamo vya kutengeza juisi za matunda kwa kutumia malighali ya mazao ikiwemo matunda yanayotokana na mabibo ya mikorosho.

"Nichagueni kwa kunipa kura za kutosha ili nianzishe viwanda vya kusindikiza mazao, hii itainua uchumi wenu katika mikoa ya kusini ikiwamo hapa wilayani Masasi na pia nitaongeza thamani ya zao la korosho ili iwe na bei ya juu," alisema Lipumba.

Alisema wakulima wa korosho katika mikao hiyo wameendelea kuwa masikini licha kulima korosho kwa miaka mingi kutokana na bei inayolipwa kwa wakulima kuwa ndogo.

Alisema bei hizo zimeendelea kumgandamiza mkulima na kuendelea kuwa masikini, lakini kupitia viwanda hivyo iwapo CUF ikipata ridhaa ya kuongoza nchi kitahakikisha inaongeza thamani na uchumi wa kusini unaimarika zaidi.

Kwa mujibu wa Prof. Lipumba, mazao mengine ambayo serikali ya CUF ikiingia madarakani pia itayaongezea thamani ni mbaazi, choroko na ufuta lengo likiwa ni kumuinua mwananchi.

Aidha, Lipumba alisema atatumia rasilimali ya gesi katika kukuza uchumi wa kusini kwani rasilimali hiyo kwa sasa haitumiki vizuri licha ya kuwa muhimu kwa kusini.

Habari Kubwa