Lissu atoa neno Membe upinzani

14Jul 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu atoa neno Membe upinzani

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amezungumzia uamuzi wa Benard Membe kujiunga na upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika awamu iliyopita ya serikali, tayari ameshatangaza kujiunga na upinzani na mwishoni mwa wiki alikuwa na mazungumzo na uongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo ambako inadaiwa atawania kiti cha urais kupitia chama hicho.

Juzi, Nipashe ilizungumza na Lissu kwa mtandao akiwa nje ya nchi, akisema kutua kwa Membe upinzani kipindi hiki hakuwezi kuvuruga mipango ya vyama vya upinzani. "Membe hawezi kuleta mgawanyiko wowote.Yeye ni mwanachama mpya wa ACT, siyo wa CHADEMA.

Hawezi kuleta mgawanyiko kwetu (CHADEMA)," Lissu alisema. Lissu anayesifika kutokana na utaalamu wake katika tasnia ya sheria, pia alizungumzia mchakato wa kumpata mgombea wa urais kupitia CHADEMA, akisema atampa ushirikiano mgombea atakayepitishwa ikiwa chama kitaona yeye hafai kupeperusha bendera yake.

"Kwanini (watia nia wengine) wanipe tabu kaka Enock (mwandishi)? Hatugombani, tunatafuta mwanachama anayeweza kustahimili mapambano makali yaliyoko mbele yetu. "Inawezekana kabisa kaka Enock nisiwe mimi.

Wapo watia nia 11 na mimi ni mmoja tu miongoni mwao," Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika alisema.

Lissu, yuko nje ya nchi tangu usiku wa Septemba 7, 2017 aliposafirishwa kwa dharura kwenda jijini Nairobi, Kenya na baadaye Ubelgiji kupata matibabu ya kibingwa kutokana na kushambuliwa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.

Hadi mwishoni mwa wiki, wanachama sita wa CHADEMA, akiwamo Lissu, walikuwa wamechukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. Mbali na Lissu, wengine ni Dk. Mayrose Majinge, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu, Wakili Gaspar Mwalyela, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita na Leonard Manyama.

Habari Kubwa