Lissu aahidi kuubadili mfumo wa elimu

26Oct 2020
Christina Mwakangale
Nipashe
Lissu aahidi kuubadili mfumo wa elimu

MGOMBEA urais wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania, atabadili mfumo wa elimu kwa kuhakikisha zinajengwa shule mpya, vyoo pamoja na nyumba za walimu.

MGOMBEA urais wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Lissu aliyasema haya kwenye mkutano wa kampeni mjini Songea mkoani Ruvuma, akisema pamoja mwamko serikali kutolewa wa uandikishaji wanafunzi shuleni, ujenzi wa miundombinu umekuwa duni kuendana na ongezeko la wanafunzi.

“Madarasa ya shule za msingi hasa mijini yamefurika wanafunzi, darasa ambalo wizara ya elimu inasema ni wanafunzi wastani 45, kuna madarasa ya wanafunzi 200, 150 au 100.

Kwa sababu tumepanua wigo wa kuingiza wanafunzi shuleni, hatujajenga madarasa, hatujajenga shule mpya na vyoo vya walimu, vyoo tulivyonavyo ni vya enzi ya Mwalimu,” alisema Lissu na kuongeza kuwa wana mpango mkubwa wa kufanya mabadiliko kwenye elimu yetu.

Alisema mabadiliko katika elimu yatakwenda sambamba na kubadili mtazamo wa elimu kwamba baadhi ya wazazi akitaka kumpeleka mwanawe shuleni, huangalia inayofaulisha.

“Sasa hivi mzazi ukitaka kumpeleka mtoto wako sekondari unajiuliza shule ipi inapasisha, tunachoangalia ni kupasi mitihani, akiwa shule msingi tunampeleka ‘tution’ (masomo ya ziada) sekondari ‘tution’, chuo kikuu ‘tution’,” alisema na kuongeza:

“Falsafa hii imejenga taifa la watoto wanaofaulu mitihani na si kufaulu maisha, kuajiriwa popote duniani…hii inawezekana, lazima tubadili mfumo wa elimu ili tusiwe na taifa la wenye ufaulu tu, bali watu wenye maarifa.”

Alisema mfumo ulipo unawafanya wahitimu wa Tanzania kuwa na ushindani mdogo kwenye soko la ajira, hususan kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Yote hii ipo katika mambo makuu, uhuru, haki na maendeleo ya watu.”

Aidha, akizungumzia kuhusu sekta afya, Lissu alisema CHADEMA itakaposhinda itahakikisha kila Mtazania anakuwa na bima ya afya, ili kupunguza gharama za matibabu.

“Matibabu yana gharama kubwa, fikiria ukilazwa hospitali zetu kwa wiki moja ni shilingi ngapi?” Alihoji.

“Kitu ambacho kinahitajika nchi hii, hakuna mwenye uwezo wa kujitibu mwenyewe hakuna, ugonjwa haubishi hodi kwamba nakuja wiki ijayo.

Bima ya kila mtu itasaidia kwa kuwa hatuugui wote kwa pamoja, ile pesa tuliyochangia itasaidia, tutanunua dawa, tutalipa wauguzi wetu, mchakato utachukua muda, lakini lazima tuanze.”

Habari Kubwa