Lissu aanika kinachomkwamisha kurejea

19Mar 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu aanika kinachomkwamisha kurejea

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amezungumzia kurejea kwake nchini kuwa kutategemea majibu ya serikali kwa Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, picha mtandao

Kamati hiyo iliiandikia barua serikali ya Tanzania kuomba kuruhusiwa kumsindikiza Lissu kurejea nchini.

Awali, kamati hiyo ilitoa mapendekezo pamoja na mambo mengine kumsindikiza kiongozi huyo kurejea nchini kutokana na hofu ya usalama wake.

Akizungumza na Nipashe juzi, Lissu ambaye kwa sasa yuko Ubelgiji alikokwenda tangu mwaka 2017 kwa matibabu akitokea Kenya alikokuwa anatibiwa baada ya gari lake kumiminiwa risasi 32 kati yake tano zilimpata mwilini. Tukio lililotokea kwenye nyumba za serikali jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Lissu, mpango wake wa kurudi uko pale pale na sasa anachosubiri ni taarifa ya majibu kutoka Kamati ya Umoja wa Mabunge Duniani.

“Bado IPU hawajanipa taarifa yoyote ya majibu ya serikali nasubiri waniambie, ndipo nitajua lini narejea nyumbani,“ alisema Lissu.

Aidha, alisema amesikitishwa na kutolewa kwa vitu ndani ya nyumba ya bunge aliyokuwa akiishi kama Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, huku akitoa lawama kwa mamlaka hizo kumzungusha aliyekwenda.

Hata hivyo, Bunge lilikanusha madai hayo kwa kueleza kuwa mtu huyo aliyetumwa na Lissu ndiye aliyekuwa hapatikani kuvitoa vitu hivyo kwenye nyumba hiyo ambayo Lissu alipangishiwa na bunge alipokuwa mnadhimu.

“Kuhusu vitu vyangu vilikwishatolewa kama wiki tatu zilizopita,” alibainisha.

Lissu alipeleka malalamiko kwa kile anachodai kutotendewa haki na Bunge la Tanzania alipovuliwa ubunge wake.

Pia aliiomba kufanyika uchunguzi wa tukio lake la kupigwa risasi Septemba, 2017 na kamati hiyo kupendekeza pamoja na mambo mengine Lissu kusindikizwa kurejea nchini.

Pamoja na pendekezo hilo la kusindikizwa, kamati hiyo imeomba maelezo kutoka Bunge la Tanzania kuhusu sababu na hoja za uamuzi wa kuvuliwa ubunge kwa Lissu kuomba ruhusa ya kutembelea Tanzania kama ilivyopendekezwa huku ikieleza kusikitishwa na jaribio la mauaji ya mbunge huyo na suala la kuvuliwa kwake ubunge.

Lissu alivuliwa ubunge wa Singida Mashariki mwaka jana na Spika Job Ndugai kwa kile kinachodaiwa kuwa ni utoro wa shughuli za bunge baada ya Spika kudai kutokupata taarifa rasmi za mahali alipokuwa Lissu.

Sababu nyingine iliyotolewa ni kutokujazwa kwa fomu za maadili ya umma kwa miaka miwili mfululizo ambazo kikawaida hujazwa na wabunge kila mwaka.

Habari Kubwa