Lissu aanza tena miujiza Ubelgiji

13Jan 2018
Mary Geofrey
Nipashe
Lissu aanza tena miujiza Ubelgiji

NI muujiza tena! Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amewashangaza tena wapendwa wake baada ya kuanza kutembea kwa kujikongoja katika wiki ya kwanza ya ngwe ya mwisho ya matibabu yake ya viungo nchini Ubelgiji.

Jumamosi iliyopita, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisafiri kwenda Brussels, Ubelgiji kwa matibabu zaidi akitokea nchini Kenya alikokuwa amelazwa kwa takribani miezi minne.

Mchana wa Alhamisi ya Septemba 7, 2017, mbunge huyo anayeshikilia pia wadhifa wa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa kupigwa  zaidi ya risasi 20 na watu wasiojulikana akiwa nje ya mahali anapoishi, Area D mjini Dodoma.

Alianza kutibiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa Nairobi, Kenya kwa matibabu Zaidi muda mfupi baadaye.

Siku moja baada ya Krismasi, maendeleo ya afya ya Lissu yalileta matumaini makubwa kwake na wapendwa wake baada ya kusimama kwa mara ya kwanza, hatua ambayo iliwaduwaza wengi pia na kuilezea kuwa ni “muujiza”.

Na sasa, mmoja wa ndugu wa Lissu, Vincent Mghwai, ameiambia Nipashe kuwa ndugu yake ameonyesha kile kinachoonekana kuwa ni muujiza mwingine baada ya kuanza mazoezi ya kutembea ikiwa siku chache tu baada ya kuwasili hospitalini nchini Ubelgiji.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Mghwai ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema kaka yake alipokewa vyema hospitalini alikolazwa hadi sasa na tayari ameanza kupata matibabu huku pia akiwashangaza kwa kuanza mazoezi ya kutembea.

“Licha ya kufika salama, (awali) alieleza kuwa amechoka sana. Alilazimika kupumzika kidogo na Jumatano alianza matibabu na kufanya mazoezi ya kutembea,” alisema Mghwai.

Ndugu huyo wa Lissu aliongeza kuwa kubwa zaidi lililowapa matumaini katika wiki ya kwanza ya kuwa kwake Ubelgiji ni hilo la kuanza kutembea kwa kukanyagia mguu ambao ndio uliojeruhiwa vibaya.

“Amefanya mazoezi na kutumia mguu wake uliojeruhiwa kutembea kwa kutumia magongo… ni mafanikio makubwa. Na baada ya mazoezi hayo, (Lissu) anatumai atapona haraka,” alisema Mghwai.

Pia alieleza kuwa, kama familia, wanaendelea kumuombea ndugu yao ili apate nafuu na kurejea nchini kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake mengine.

Awali, iliwahi kuelezwa kuwa akiwa nchini Ubelgiji, madaktari wataangalia pia uwezekano wa kuondoa risasi moja iliyonasia katika nyonga, kuangalia maendeleo ya operesheni 17 alizowahi kufanyiwa akiwa Dodoma na Nairobi, Kenya na pia kufanyishwa mazoezi ya viungo.

Kwa mujibu wa Lissu, watu waliomshambulia walimpiga risasi 16 zilizoingia mwilini, nane zikiondolewa na madaktari waliomtibu Dodoma na zingine saba zikiondolewa Kenya huku moja ikibaki mwilini baada ya kunasia kwenye nyonga na madaktari kumwambia kuwa haina madhara makubwa kulinganisha na hatari inayoweza kutokea iwapo wangejaribu kuiondoa.