Lissu agonga mwamba fidia kesi ya uchaguzi

24Nov 2016
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Lissu agonga mwamba fidia kesi ya uchaguzi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma, imetupilia mbali ombi la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kuhusu madai ya kesi ya gharama za Uchaguzi Mkuu wa 2015 Sh. milioni 105 alizokuwa akimdai Jonathan Njau baada ya kushinda kesi ya uchaguzi dhidi yake.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Machi 23, mwaka huu, Lissu alifungua kesi namba 6/2016, kudai fidia ya gharama za kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Njau.

Awali, aliyekuwa mgombea wa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jonathan Njau, alipinga ushindi wa Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisha kufungua kesi namba 1/2015 ya kupinga matokeo hayo.

Hata hivyo, Njau kupitia wakili wake, Godfrey Wasonga wa kampuni ya uwakili ya National, aliondoa kesi hiyo kwa madai hawezi kuendelea nayo, hivyo mahakama hiyo kumpa ushindi Lissu.

Baada ya uamuzi huo, Lissu alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, akidai fidia ya kiasi hicho.

Wakili wa mlalamikiwa, Wasonga, aliweka pingamizi la kupinga gharama hizo za uchaguzi, kwa madai kuwa lilikuwa nje ya muda wa kisheria.

Akisoma hukumu hiyo jana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, John Chaba, alisema maombi ya Lissu hayakuwa na msingi kwa kuwa kuna baadhi ya vifungu ambavyo vilikiukwa wakati wa kuomba madai hayo, hivyo kuitupilia mbali.

Msajili alisema kesi hiyo, iliyotajwa Septemba 28, mwaka huu, pande zote mbili zilitakiwa kupeleka hoja kabla ya Oktoba 14, 2016, lakini upande mmoja ulishindwa kutekeleza.

Chaba alisema mahakama ilizitaka pande hizo kujibu maandishi kabla ya upande wa mlalamikiwa kufanya hivyo, lakini Lissu hakuwasilisha maandishi yoyote.

Alisema hoja za upande wa utetezi kupitia wakili Wasonga zilikuwa na nguvu kisheria huku zikizingatia matakwa ya kisheria pamoja na kuwasilishwa kwa wakati kama ilivyotakiwa.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Wasonga alisema mahakama imetenda haki kwa kuifuta kesi hiyo kutokana na madai hayo kutokuwa na msingi wa sheria.

“Lissu kwa kujua hilo aliingia mitini hajaonekana mahakamani kila kesi inapotajwa, kutokana na kufahamu madai hayo hayana msingi kisheria,” alisema.

Habari Kubwa