Lissu aomba kukutana na Rais Samia

12Apr 2021
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu aomba kukutana na Rais Samia

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia chama hicho mwaka 2020, Tundu Lissu, amedokeza ombi lake la kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya mashauriano ya mambo kadhaa yanayohusu hali ya kisiasa kwa sasa.

Akizungumza jana katika mkutano wa mtandaoni na wadau mbalimbali wa siasa (zoom meeting) mwanasiasa huyo, ambaye alirejea nchini Ubelgiji baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020, alisema ameshaandika ujumbe wa ombi lake hilo kupitia kwa wasaidizi wa Rais Samia wiki mbili zilizopita na sasa anasubiri kujibiwa.

"Alipoapishwa Rais Samia kwa sababu nilifanya naye kazi miaka ile akiwa Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia masuala ya Muungano na alikuja kuniangalia hospitali Nairobi kama mtakumbuka, nikapeleka (kupiga) simu kwa msaidizi wake na kumwambia naomba Mama akipata nafasi uniambie nizungumze naye, bado nasubiri," alibainisha Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu, ili nchi iendelee, ni muhimu kukawa na uhuru wa kumshauri Rais na kumwambia ukweli pale anapokosea ili arekebishe na kumwambia anayofanya vizuri ili aongeze juhudi ya kuyafanya kuliko kujiamulia mwenyewe na hatimaye kuishia kubebeshwa lawama kila wakati.

Alisema pamoja na kwamba Rais Samia alikuwa sehemu ya serikali iliyopita kwa kuwa Makamu wa Rais katika kipindi cha Hayati Dk.John Magufuli, lakini anayo nafasi ya kufanya mabadiliko pale anapoona hapakuwa sawa kwa mustakabali wa wananchi wote badala ya kuzingatia maslahi binafsi ya viongozi wachache.

"Watu wanasema huyu Mama si alikuwa sehemu ya serikali hiyo anaweza kweli? Angola wana rais mpya mwaka wa pili sasa Eduardo do Santos alikuwa Rais wa Angola kwa miaka 40 akamuachia Waziri wake wa ulinzi na akahakikisha kwamba Waziri wa Ulinzi hawezi kumgeuka wote ni watu wa MPLA," alisema Lissu.

"Hivi tunavyozungumza binti wa Rais ambaye ndiye tajiri mkubwa Angola na vile vile ana mali nyingi kuliko Wareno wengi Ureno na ana mali nyingi kuliko Wa-Brazil wengi Brazil mali zake zote zimekamatwa na anachunguzwa na serikali ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi kwa Rais Eduardo do Santos,” alisema Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu, Katiba iliyopo Makamu wa Rais hufanya kazi anazopangiwa na Rais na pia Rais halazimiki kuchukua ushauri wa mtu yeyote, hivyo kumtetea Rais Samia kuwa hakuwa na mamlaka ya kufanya chochote hivyo sasa ni wakati wake akiwa kama Rais ana mamlaka yote ya kusafisha yaliyotokea huko nyuma.

Aidha, Lissu alikumbushia umuhimu wa kutengeneza katiba mpya ili kuwa na mfumo wa kitaasisi ambao viongozi watawajibika badala ya kudanganywa na kile kinachoitwa nia njema za viongozi ambazo baadae huja kudhihirika kuwa ni ulaghai.

Habari Kubwa