Lissu 'auziwa' kesi ya Mbunge Chadema

12Jan 2017
Ashton Balaigwa
Nipashe
Lissu 'auziwa' kesi ya Mbunge Chadema
  • Ni baada ya kufuNgwa miezi 6 bila faini

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, imemhukumu kutumikia kifungo cha miezi sita jela, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Lijualikali (30) kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki.

Hata hivyo, Mbunge wa Mikumi Joseph 'Profesa Jay' Haule (Chadema), alisema aliwasiliana na viongozi wa kitaifa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na kwamba wanakusudia kukata rufaa kupinga maamuzi hayo.

Profesa Jay ambaye jimbo lake ni jirani na Kilombero linaloongozwa na Lijualikali, alisema hukumu hiyo imemshtua.

Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Timothy Lyon alisema amemhuku kifungo Lijuakali baada ya kumtia hatiani kwa kosa yeye na dereva wake, kwa kuwa Mbunge huyo amepatikana na hatia katika kesi tatu huko nyuma na kuhukumiwa kulipa faini.
Alisema Mbunge huyo anastahili kutumikia adhabu hiyo ya kwenda jela miezi sita.

Lyon alizitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini kuwa ni namba 338 ya mwaka 2014, namba 220 ya mwaka 2014 na namba 340 ya mwaka 2014.

Alisema Mahakama kwa kuona mshtakiwa ni mhalifu mzoefu na imeona adhabu yake iwe kifungo cha miezi sita jela.
Hata hivyo, mahakama hiyo imeona kwa kuwa mshtakiwa wa pili Stephano Mgata(35) ni mara yake ya kwanza kutenda kosa inamhukumu kifungo cha miezi sita nje.

Ndani ya kipindi hicho cha miezi sita Mgata hatotakiwa kutenda kosa lolote la jinai.

Wakati wa hukumu hiyo ikisomwa hali katika mahakama hiyo ilikuwa tulivu tofauti na kesi zilizopita kutokana na wafuasi wa Chadema kuwa wachache licha ya kusambazwa kwa ujumbe wa kuwataka wafike kwa wingi siku ya hukumu.

Katika Eneo la Mahakama hiyo kulikuwa na polisi wachache wakiendelea shughuli zao.

Baada ya hukumu kutolewa Mbunge huyo alipelekwa haraka gerezani ili kuanza kutumikia kifungo chake.

Viongozi wa Chadema walisema wanawasiliana na viongozi wa makao makuu ya chama Dar es Salaam ili kushughulikia kadhia hiyo.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Shaban Mikongole alisema hawakuridhika nayo na kwamba wanawasilianza na wakili aliyesimamia kesi hiyo pamoja na wanasheria wa chama hicho ili kuweza kukata rufaa.

Aliwataka wanachama wa Chadema kuwa watulivu katika kipindi hiki licha ya kutoridhishwa na hukumu hiyo iliyotolewa, kwa kuwa suala hilo litashughulikiwa na uongozi wa taifa kwa pamoja na mkoa na wilaya.

Awali, mwendesha mashtaka Inspekta wa Polisi, Dotto Ngimbwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na Mgata walitenda kosa hilo Machi mosi mwaka 2016 eneo la Kibaoni katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

Ngimbwa alisema washtakiwa hawa kwa pamoja walifanya fujo kinyume cha sheria.

Alisema mnamo Machi mosi mwaka 2016 saa 4 asubuhi maeneo ya Kibaoni katika maeneo ya ukumbi wa Halmashauri washtakiwa walifanya fujo na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Washtakiwa walikana mashtaka lakini upande wa mashtaka ukathibitisha bila kuacha shaka, kwa mujibu wa mahakama.

Habari Kubwa