Lissu azigeukia hifadhi za taifa

16Sep 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu azigeukia hifadhi za taifa

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema akipewa ridhaa ya kuongoza nchi, ataweka utaratibu mpya wa hifadhi za taifa ili uwapo wake uwe unapewa baraka na wananchi.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika viwanja vya National Housing mjini Njombe jana. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Lissu aliyasema hayo jana wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni mkoani Mbeya, akisisitiza kuwa ni lazima wananchi wakubali kwanza kuwa na hifadhi eneo husika.

Alisema sheria za kimataifa kuhusu masuala ya uhifadhi zinataka kuwe na ridhaa ya wananchi kuhusu miradi wanayopelekewa na serikali inayoathiri maslahi yao.

“Nani atakayeathiriwa na hiyo mipaka, atalipwaje fidia, akiondolewa atapelekwa wapi? Baada ya hayo yote ndipo waamue wanataka au hawataki, wakisema hawataki, mwisho wa habari,” alisema.

Lissu alisema iwe katika kujenga barabara, kupanua shule, kujenga hifadhi, uamuzi unaothiri haki za watu, lazima wananchi watoe ridhaa yao baada ya kupata taarifa zote za mradi husika.

“Tutaitoa kwenye sheria za kimataifa na kuiweka kwenye katiba yetu, ukweli ni kwamba Jaji Joseph Warioba alituasia sana, mapendekezo mengi yapo kwenye mapendekezo ya tume ya Jaji Warioba.

“Wanafikiri maendeleo ni yale yanayotumia nguvu, sisi maendeleo ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliandika kwenye kitabu chake ni yale ambayo hayatumii nguvu, ndiyo maana tunazungumza uhuru, haki na maendeleo ya watu.

“Tuna hifadhi za taifa zaidi ya 20, maana yake ni nini? Ukitengeneza hifadhi ya taifa unafukuza watu kwenye maendeleo, ukienda kwenye maeneo yote yenye hifadhi ya taifa ni vita na wenyeji,” alisema.

Lissu pia aliahidi kuweka mfumo mpya wa kodi ili kile alichokiita mvutano kati ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na wafanyabiashara ukome.

"Kufilisi watu na kuwabambika kodi kubwa tutayamaliza, tutaleta mfumo wa haki ya mlipakodi, kabla ya kukuambia chochote lazima akwambie una haki gani, kama anakudai, lazima aweke utaratibu wa kulipa ili usiue biashara yako kwa sababu ikifa, wanaoathirika ni wengi," alisema.

Lissu pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia msaada wa kukodiwa ndege kwenda Nairobi kutibiwa, aliopewa na aliyekuwa Mbunge wa Mpendae, Salim Turky, ambaye alifariki dunia usiku wa jana.

Habari Kubwa