Lissu kufuta vitambulisho vya machinga

06Sep 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe Jumapili
Lissu kufuta vitambulisho vya machinga

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameahidi kufuta utaratibu wa serikali kutoa vitambulisho maalum kwa wafanyabiashara ndogo, maarufu machinga, ikiwa atashinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu akiwapungia mkono wanachama na wafuasi wa chama hicho, alipowasili katika viwanja vya Nzovwe, jijini Mbeya jana, kwa ajili ya mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu. PICHA: NEBART MSOKWA

Lissu alitoa ahadi hiyo jana kwenye Uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini hapa wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho Kanda ya Nyasa, akiahidi kujenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kundi hilo ambayo yatakuwa wazi usiku na mchana.

Lissu alisema baadhi ya wananchi huwa wanachelewa kufika kwenye miji yao wanapokuwa wametoka safarini na hivyo kukosa huduma za kununua mahitaji kwenye masoko kutokana na masoko hayo kufungwa kwa kisingizio cha usalama.

“Tutafuta utaratibu wa kuwauzia wamachinga vitambulisho ambavyo vinatolewa sasa. Pamoja na kupewa vitambulisho hivyo, wanauza bidhaa zao kwenye mitaro na barabarani, jua linakuwa lao na mvua yao.

“Tutajenga masoko maalum kwa kushirikiana na sekta binafsi kwenye maeneo mbalimbali ili machinga wetu wafanye biashara hapo kwa uhuru na kila mmoja atakuwa na chumba chake,” aliahidi.

Vilevile, Lissu alisema serikali yao itajenga majengo maalumu kwenye maeneo ya stendi za mabasi kwa ajili wa wauzaji vyakula, maarufu mamalishe na babalishe, ili wafanyie biashara zao huko kwa uhuru.

Mgombea huyo pia aliahidi kuwa serikali yake haitakuwa ya kulipa kisasi kwa mtu yeyote na badala yake ataunda tume ya maridhiano ambayo itakuwa kwa ajili ya upatanishi wa Watanzania na viongozi wote ambao walifanya makosa watatakiwa kukiri makosa yao na watasamehewa.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alivitaka vyombo vya dola na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuvitendea haki vyama vyote vya siasa wakati huu wa uchaguzi.

Alisema NEC inapaswa kutenda haki hiyo kwa kuwarejesha kwenye mchakato wagombea ubunge na udiwani wa vyama vya upinzani walioenguliwa na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi.

Habari Kubwa