Lissu: Nitawarejeshea haki waliodhulumiwa

08Sep 2020
Rahma Suleiman
 ZANZIBAR
Nipashe
Lissu: Nitawarejeshea haki waliodhulumiwa

MGOMBEA urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu, aliahidi endapo atapata urais atahakikisha anairejesha haki ya Wazanzibari kwa wale wote waliodhulumiwa.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akiwasili katika viwanja vya Kibandamaiti, Unguja jana, kwa ajili ya kuhutubia katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu. PICHA: RAHMA SULEIMAN

Alitoa ahadi hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, ambapo alisema kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye anayeweza kuking'oa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alidai kuwa maamuzi makubwa ya kisiasa kuhusu Zanzibar hufanyika Tanzania Bara.

Alisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu wapinzani wana uwezo wa kuishinda, lakini ni lazima wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara wakafanya uamuzi mgumu.

Alisema kuna haja kwa vyama vingine vya siasa kumuunga mkono Maalim Seif, ambaye ana uwezo wa kuishinda CCM.

Alisema maslahi ya Wazanzibari katika uchaguzi wa mwaka huu ni kumuunga mkono Maalim Seif.

Alisema kumuunga mkono mgombea huyo wa ACT haina maana kuwa wanawasaliti wagombea wao.

Alisema kwa upande wa urais wa Tanzania, CHADEMA ina uwezo wa kushinda, hivyo vyama vingine havinabudi kuiunga mkono.

 Anayeiweza kuishinda CCM ni CHADEMA hivyo ni vyema kukiunga mkono.

Kadhalika, Lissu alieleza kuwa lazima yafikiwe maridhiano ya kitaifa ili kusameheana na kuunda kwa tume huru ya katiba.

Aidha, alisema watapigania haki ili Taifa liinuke na hawatakuwa tayari kuibiwa kura katika uchaguzi wa Oktoba.

Naye mgombea mwenza wa CHADEMA, Salum Mwalimu Juma, alisema kuwa watakaposhinda atahakikisha anamshauri Rais kuwatoa mahabusu viongozi wa Jumuiya ya  Uamsho.

Aidha, Mwalimu alisema mambo muhimu watakayoyafanyia kazi watakapoingia madarakani ni kuipatia mamlaka kamili Zanzibar, kulipa fidia mauaji ya Wazanzibari yaliotokea Pemba mwaka 2001.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema ili kupata uchaguzi huru na haki, lazima kuwapo haki.

Habari Kubwa