Lissu, Nyalandu, Majinge wapenya urais CHADEMA

04Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu, Nyalandu, Majinge wapenya urais CHADEMA

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imepitisha majina matatu ya watiania wa urais kupitia chama hicho.

Waliopitishwa ni Dk. Mayrose Majinge, Lazaro Nyalandu na Tundu Lissu, kati ya wagombea saba waliotia nia ambao Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la CHADEMA uliyapigia kura na kupata mgombea mmoja.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alitangaza majina ya watiania waliopitishwa jana jijini Dar es Salaam, mbele ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.

Alisema jina moja lililopitishwa na Mkutano huo Mkuu wa Baraza Kuu, litapitishwa na Mkutano Mkuu wa CHADEMA utakaofanyika leo.

Wagombea hao watatu walipata fursa ya kujinadi na kujieleza mbele ya mkutano huo na kuulizwa maswali na wajumbe kabla ya kuwapigia kura.

MBOWE AELEZA ALIVYOKACHA URAIS

Kwa upande wake, Mbowe alieleza sababu za kutotangaza nia ya kuwania kinyang’anyiro hicho, licha ya kuchukuliwa fomu na baadhi ya wanachama.

Katika mchakato huo, wanachama 11 walichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho akiwamo Mbowe, lakini ni wanachama saba tu ndio waliorudisha na kutangaza nia.

Mbowe alisema alikacha mbio za kugombea urais wa Tanzania ili akijenge chama hicho.

Alisema tamaa zake haziwezi kuwa na thamani, ikilinganishwa na thamani ya CHADEMA.

“Nilifuatwa nikaambiwa mwenyekiti gombea urais, nikakubali, lakini sikutangaza nia. Hofu ikaibuka mwenyekiti anagombea,
makamu anagombea, nikasoma kwenye mitandao, lakini mimi binafsi kama Mbowe hiki chama kwangu ni kama mtoto, haiwezekani tamaa zangu binafsi zikawa za maana kuliko uhai wa chama chetu,” alisema.

Mbowe alisema hatoiacha safari ya kuijenga CHADEMA kwa sababu ya maslahi yake binafsi. “Tumeamua sana kuijenga CHADEMA, hatutaiacha safari hiyo kwa sababau ya maslahi binafsi,” alisisitiza Mbowe.

Kadhalika, Mbowe aliwataka wajumbe kuchagua mgombea anayefaa na kuepuka mipasuko.

“Nguvu yetu ni umoja wetu, tutoke hapa wote tuna nyuso za furaha, tumpate mgombea katika mazingira ya kuujenga umoja wetu na siyo mpasuko kati yetu,” alisema.

Mbowe pia aliwasihi wajumbe wa baraza hilo kutowabagua Wana-CHADEMA waliowahi kuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tunahitaji kuonyesha upendo ndani ya chama chetu kuimarisha Tanzania kujenga umoja wetu, hatuhitaji kufanya makosa ya CCM kutubagua na sisi tukafanya ubaguzi dhidi ya wanachama wenzetu kwa sababu walikuwa CCM, tunahitaji umoja wa kitaifa, tunahitaji mtu mmoja,” alisema.

USHIRIKIANO NA ACT-WAZALENDO

Kadhalika, Mbowe alisema CHADEMA inaendelea kufanya mazungumzo na Chama cha ACT-Wazalendo, kwa ajili ya kuunda nguvu moja ili kuing’oa CCM madarakani.

Alisema CHADEMA na ACT-Wazalendo kwa sasa vinapanga mashambulizi ya kisiasa dhidi ya CCM.

“Hatutaingia kwenye ushirikiano kama fasheni, tutaingia kwenye ushirikiano kama kuna watu wako makini, ambao hawatatuuza njiani, tunakubaliana jamani?” Alihoji Mbowe huku akishangiliwa.

Aliendelea: “Tunaendelea na mazungumzo, lakini niseme bayana, katika mazungumzo tunayoendelea nayo, tunaendelea na mazungumzo na Chama cha ACT-Wazalendo.”

Alisema kuhusu mategemeo ya maongezi yao inatategemea mawazo ya kila mmoja, na kwamba pia watazungumzia kuachiana nafasi ya urais Zanzibar.

Mbowe alisema katika mazungumzo hayo, CHADEMA iko tayari kuachia nafasi za kugombea.

“Huko nyuma tuliingia kwenye mazungumzo ya ushirikiano wa vyama vingine, miongoni mwa sababu ni unyonge wa chama chetu katika baadhi ya maeneo, lakini leo tunashirikiana na vyama vingine kwa sababu kuna maeneo vyama vingine vina nguvu kuliko wagombea wetu,” alisema Mbowe.

Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA kinaweza kuwa chama kikubwa, lakini kinapaswa kuheshimu mawazo ya chama kingine ambacho kinataka kushirikiana nacho.

“Tumheshimu kila mwenzetu kwa ukubwa wake, ukubwa wetu utujengee unyenyekevu usitujengee kiburi, tunapoona kuna sababu ya kushirikiana, tutashirikiana na tukiona hakuna maslahi mapana ya chama na taifa letu, tutafikiria tofauti,” alisema Mbowe.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, vyama vya upinzani viliunda ushirikiano uliounda umoja uliotokana wakati wa Bunge la Katiba na kuitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kumsimamisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, aliyechuana na Rais John Magufuli.

Habari Kubwa