Lissu, Prof. Lipumba wakutana uwanja mmoja kufanya kampeni

23Sep 2020
Lilian Lugakingira
KAGERA
Nipashe
Lissu, Prof. Lipumba wakutana uwanja mmoja kufanya kampeni

Wagombea kiti cha urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamegongana katika eneo moja la mkutano katika viwanja vya Fatuma wilayani Muleba mkoani Kagera.

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa leo Septemba 23,2020 kwa ajili ya Lissu lakini kabla ya Lissu kufika alifika Lipumba na kuanza kuhutubia wananchi, hali iliyomfanya Lissu kuondoka eneo hilo baada ya kumkuta Lipumba.

Ratiba ya Lissu kufanya mkutano katika eneo hilo ilikuwa ya jana Septemba 22,2020 lakini kutokana na msafara wake kuchelewa kutoka Wilaya ya Karagwe, uliahirishwa hadi leo saa mbili asubuhi, ambapo wananchi walikwishajitokeza kumsubiri.

Lipumba alifika katika eneo hilo akitokea Rulanda wilayani Muleba, na kutokana na kukuta maandalizi ya CHADEMA, CUF walitandika kitambaa chao mezani lakini bendera za CHADEMA ziliendelea kupeperuka, naye akahutubia wananchi walijitokeza.

Habari Kubwa