Lowassa afunguka kurudi nyumbani

04Mar 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lowassa afunguka kurudi nyumbani

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amesema ataweka wazi sababu zilizomwondoa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

Ijumaa, Lowassa ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitangaza kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kurejea chama tawala akipokewa na viongozi wakuu wa CCM walioongozwa na Mwenyekiti, Dk. John Magufuli.

Muda mfupi baada ya kupokewa na uongozi wa CCM, Lowassa alipewa fursa ya kuzungumza, lakini alisema maneno machache tu kuwa "nimerudi nyumbani".

Hata hivyo, kumekuwa kukielezwa sababu nyingi zinazodaiwa na wadau wa siasa nchini kwama zimemsukuma Lowassa kurejea CCM.

Kutokana na hali hiyo, Nipashe jana ilimtafuta Lowassa kujua sababu za kukihama chama kilichompa nafasi ya kukiwakilisha kusaka kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika mazungumzo hayo na Nipashe, Lowassa hakuwa tayari kuweka bayana sababu zilizomsukuma kurejea CCM, lakini alisisitiza kuwa wakati wowote kuanzia sasa, atazungumzia suala hilo kwa kina atakapokutana na waandishi wa habari.

“Nimepanga wakati wowote kuzungumzia kitendo changu cha kuondoka kwangu Chadema na kurudi CCM, maswali yote uliyonayo, nitayajibu kupitia mkutano huo wa waandishi wa habari,” Lowassa alisema.

Nipashe ilipotaka kujua siku ya kufanyika kwa mkutano huo wa Lowassa na waandishi wa habari, Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alijibu: "Wakati wowote kuanzia sasa, mtaarifiwa kuhusu mkutano wangu, usiwe na wasiwasi utajulishwa, nitazungumza yote unayoyahitaji kuhusu mimi."

Lowassa alipokewa na viongozi wa CCM kwenye ofisi ndogo zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam, ikiwa ni takribani miaka minne tangu akihame Julai 2015, baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia chama hicho.

Wengine waliokuwapo kwenye mapokezi hayo ya Lowassa ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.

Pia picha zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii Ijumaa, zilionyesha Lowassa akiwa ameongozana na mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz.

Akitangaza uamuzi huo wa Lowassa kurejea CCM, Dk. Bashiru alisema mwanasiasa huyo mzoefu ameamua kurejea chama tawala kuanzia siku hiyo.

“Lowassa amerejea nyumbani, kwa hiyo tunaanza kazi ya kujenga taifa letu na kulinda uhuru wetu,” Dk. Bashiru alisema na kuongeza kuwa: "Lowassa ameamua kuweka siasa pembeni na kuungana na Rais Magufuli kuliletea taifa maendeleo."

Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, akihojiwa na kituo cha runinga cha ITV, alidai Lowassa aliomba kurudi CCM na walimjadili kwa saa nne.

Alisema alifika kwenye Ofisi za CCM Ijumaa kwenye vikao vya uongozi vilivyokuwa vikiendelea na kueleza uamuzi wake na kwa kuzingatia taratibu alizoeleza, waliamua kumpokea.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kuhamia upinzani katika historia ya Tanzania, alitangaza kujiengua CCM Julai 28, baada ya jina lake kushindwa kupenya katika majina matano yaliyoteuliwa na Kamati Kuu ya CCM, kuwania urais katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Katika uchaguzi huo, Lowassa aligombea nafasi ya urais kupitia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD na kupata kura 6,072,848 (sawa na asilimia 39.97) akiwa nyuma ya Dk. Magufuli aliyetangazwa mshindi kwa kupata kura 8,882,935 (asilimia 58.46).

Lowassa alitangaza kukihama chama hicho, alinukuliwa akisema: “Kikatiba, Kamati ya Maadili ya CCM iliyokata jina langu na majina mengine, haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea urais kupitia CCM, lakini ilifanya hivyo.”