Lowassa amfagilia Trump

02Jan 2017
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Lowassa amfagilia Trump

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewapongeza Wamarekani kwa kumchagua Donald Trump, kuwa Rais wao akisema ni shupavu, mwenye uwezo na maamuzi magumu.

Lowasa aliyasema hayo jana katika misa maalum ya shukrani na kuuombea mwaka mpya wa 2017 iliyoshirikisha madhehebu mawili ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli na Kanisa Katoliki wilayani humo.

Misa hiyo ya shukrani ilifanyika katika Kanisa la KKKT Jimbo la Maasai wilayani Monduli na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo wakiwamo viongozi wa chama na serikali wa ngazi mbalimbali.

Pia Lowassa aliwataka wananchi kuacha kulalamika na badala yake wafanye kazi kweli kweli kwani ndiyo njia sahihi ya kuondokana na taifa maskini.

Alisema Wamarekani hawakufanya makosa kumchagua Trump kwani ameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza taifa hilo tajiri na lenye nguvu duniani.

Lowassa ambaye alipewa nafasi ya kusalimia waumini wa madhehebu hayo kutokana na kutoonekana kwa muda mrefu katika jimbo hilo, alisema kwa sasa anafanya siasa za kimataifa zaidi tofauti na watu walivyozoea kumwona majukwaani.

"Dunia imebadilika, Wamarekani wamemchagua Rais mwamba kweli kweli, hatuwezi kumtabiria mambo yake yatakavyokuwa, ila ninachowaomba mchape kazi kweli kweli ili kuondokana na umaskini," alisema Lowassa.

Pia aliwataka viongozi waliochaguliwa kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua huku akimtaka Meya wa Jiji la

Arusha, Calist Lazaro na Mwenyekiti wa Halmashuri ya Monduli, Isaac Joseph, kuzingatia miradi inayopitishwa inawanufaisha wananchi kwa asilimia 100.

Habari Kubwa