Lowassa awashukuru Wazanzibari kwa mahaba

09Jan 2017
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Lowassa awashukuru Wazanzibari kwa mahaba

ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu mwaka juzi, Edward Lowassa, amewashukuru Wazanzibar kwa mahaba yao ya kumpa kura wakati wa uchaguzi huo.

Lowassa aliyasema hayo alipohutubia uzinduzi wa kampeni za ubunge Jimbo la Dimani, katika viwanja vya Fuoni visiwani humu jana, akiwa na viongozi kadhaa waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwamo Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Nawashukuru sana kwa mahaba yenu kwani yameonekana. Wazanzibar ahsanteni sana,” alisema Lowassa ambaye wakati wa uchaguzi mkuu huo, aliungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mbali ya Chadema, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

“Baada ya uchaguzi, tulizuiwa kufanya mikutano, lakini Maalim Seif alifanya kazi kubwa sana, wakizuia huku, alikuwa anapita njia nyingine, walikuwa wanamfuata kila mahali hata misikitini, lakini hawamuwezi,” alisema Lowassa.

Alimpongeza Maalim Seif kwa kumualika katika mkutano huo wa uzinduzi kwa kuwa alipanga kuja mapema Zanzibar kuwashukuru kwa kupigiwa kura nyingi kuzidi wagombea wengine.

Hata hivyo, Lowassa alisema alishindwa kuja visiwani humu kwa kuwa mikutano ya hadhara ilizuiwa kwa vyama vya siasa.

Aliwataka wana-Ukawa sasa kuanza kujipanga kikamilifu kwa uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020.

MAALIM SEIF AMJIBU KINANA
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif amewataka wanachama wa chama hicho kupuuza kauli zilizotolewa visiwani humu hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Maalim Seif alisema wanachama wa CUF walivunjika moyo kutokana na kauli ya Kinana aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano wao wa kampenni hivi karibuni visiwani humu.

“Wengi wametishika na kauli ya Kinana…hajui chochote kinachoendelea katika nchi na hata katika chama chake, mwacheni mwenyewe,” alisema Maalim Seif.

AELEZA USHIRIKI WA CUF
Maalim Seif alisema CUF inashiriki uchaguzi huo wa Jimbo la Dimani kwa kuwa uko tofauti na ule wa marudio.

Alisema uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani upo kwa mujibu wa Katiba kwa sababu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haikufuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi na walitangaza matokeo na imeitisha uchaguzi mdogo kwa mujibu wa Katiba.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Abdulrazak Khatib, aliwaomba wananchi kumpigia kura ili ashughulikie kero nyingi zinazowakabili.

Mkutano huo ulihudhuriwa na umati wa wafuasi wa CUF ambao muda wote walikuwa wakiimba nyimbo zenye ujumbe wenye kumpamba Maalim Seif.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Januari 22 kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir (CCM), kufariki dunia Novemba mwaka jana mjini Dodoma.

Habari Kubwa