Akizungumza na washiriki wa mkutano huu uliofanyika kwa njia ya mtandao, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema mkutano huu unafanyika mahususi kwa ajili ya kuweka mipango mikakati wa kuendelea kufanya kazi pamoja kati ya LSF na wadau wake wote wa masusala ya haki na hasa mashirika ya wasaidizi wa kisheria katika kipindi hiki cha mwaka 2021.
“Nina furaha sana kuonana nanyi leo. Ingawaje mko mbali lakini kupitia teknolojia tunaweza kukutana na kujadili maswala muhimu katika mustakabadhi mzima wa upatikanaji wa haki. Nina furaha zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wadau wetu nyinyi mmefanya kazi kubwa sana na imetupa matokeo makubwa ukilinganisha na malengo tuliyokuwa tumejiwekea,” amesema Ng’wanakilala.
Akinukuu takwimu kutoka katika ripoti ya LSF ya mwaka 2020, Ng’wanakilala amesema kuwa wadau wa LSF wamefanikiwa kutoa elimu ya masula ya kisheria iliyowafikia watu takribani million 6.4, ambapo asilimia 45 walikuwa wanaume na asilimia 55 walikuwa wanawake.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu kazi zinazofanywa na wadau wetu. Tunatumia taarifa hizi kwa ajili ya kupanga mikakati mizuri ili kuweza kuwafikia watu wengi hasa wenye uhitaji kama vile wanawake na watoto. Lengo letu ni kuleta maendeleo kwakuwa tunaamini kabisa hakuna maendeleo bila haki,” amesema Ng’wanakilala.
Ameongeza kuwa LSF imeandaa mkutano huo maalum kwa ajili ya kukutana na wadau wake ambao ni mashirika zaidi ya 200 ya wasaidizi wa kisheria nchi nzima pamoja na mashirika yanayotekeleza miradi ya upatikaji wa haki mijini ili kujadili masuala ya kiutendaji katika suala zima la utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji hususani wanawake na watoto.
Amefafanua kuwa mkutano huo ni sehemu ya majukwaa mbalimbali ambayo LSF huandaa kila mwaka ili kukutana na watendaji wakuu wa mashirika ya wasaidizi wa kisheria maarufu kama ‘Paralegals’ ikiwemo wakurugenzi wakuu wa mashirika na watendaji wengine wa mashirika haya ili kuangalia maeneo muhimu ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa haki nchini.

"Ikumbukwe kuwa LSF imekuwa ikitekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini katika kipindi cha takribani miaka 10, ambapo imekuwa ikitoa ruzuku kwa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria ili kusaidia watu mbalimbali hasa wanawake" amesema
Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Bumbuli (BPO) mkoani Tanga, Ramadhani Mtana, ameishukuru LSF kwa kazi kubwa ya kuendelea kutoa ruzuku kwa wadau wake na hasa wasaidizi wa kisheria kwakuwa suala la fedha limekuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“LSF kama wadau wetu mkuu tunakushukuru sana kwani umekuwa mstari wa mbele kutoa mchango wako hasa ruzuku katika taasisi zetu. Kupitia ruzuku hizi tumeweza kuhudumia wananchi wengi nchini hasa wanawake ambao wanakumbana na changamoto mbalimbali kama vile kesi za mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na matatizo mengine,” amesema Mtana.

LSF kupitia wadau watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria mpaka sasa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imesaidia kutolewa kwa elimu ya masuala ya kisheria, jambo lilisababisha kuripotiwa kwa matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia, ambapo asilimia 68 ya matukio yote yaliyoripotiwa yalitatuliwa na wasaidizi wa kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani, asilimia 11 ya matukio yaliyoripotiwa yalipewa rufaa ya kwenda mbele kwa hatua zaidi na asilimia 17 ya matukio yaliyoripotiwa bado yanashughulikiwa mpaka sasa.
