LSF yakutana na wadau kutathimini programu ya upatikanaji haki

22Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
LSF yakutana na wadau kutathimini programu ya upatikanaji haki

MKURUGENZI wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Visiwani Zanzibar,Hanifa Ramadhan Said amesema kupitia programu ya Shirika la Legal Services Facility (LSF) na wadau wake nchi nzima kumewezesha kwa kusaidia jamii kupitia uwezeshaji wa kisheria.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng'wanakilala akizungumza na wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria.

Aidha LSF imesaidia kuundwa na kupitisha kwa sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017 iliyofanya kazi za watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kutambulika.

Kauli hiyo ameitoa jana Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa siku mbili uliofunguliwa Oktoba 21,2021 hadi jana ambao ulikutanisha wadau wake kutoka Tanzania Bara na Visiwani kufanya tathimini ya utekelezaji wa program ya upatikanaji haki kwa mwaka 2021.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Hanifa, amesema mkutano huo ni muhimu kwakuwa unawaleta pamoja wadau msaada wa kisheria ambao wamekuwa ni sehemu kubwa ya mafanikio katika kukuza upatikanaji wa haki nchini.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe akizungumza na wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 - 21 Oktoba 2021.

Amesema moja ya mafaniko ni kushirikiana na jeshi la polisi kuwasapoti kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 400 ili wapitie mwongozo wa jeshi lao (PGOs) na hiyo kuwa fursa ya kurasimisha rasmi uwepo wa madawati wa wanawake na watoto katika vituo vya polisi.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta ya msaada wa kisheria.  Kumekuwa na taabu mbalimbali katika jamii ambazo husababishwa na ukandamizaji wa haki mbalimbali ikiwemo wanawake na watoto. Kupitia programu ya LSF na wadau wake nchini mmeweza kufanya kazi kubwa ya kusaidia jamii kupitia uwezeshaji wa kisheria.” amesema

Amesema kuwa mkutano huo ulijumuisha washiriki takribani 200 ikiwemo watendaji wakuu wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kutoka mikoa yote nchini Tanzania. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng'wanakilala akizungumza na wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 200 kutoka Tanzania nzima wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa LSF uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 - 21 Oktoba 2021.

Ameongeza kuwa mkutano huo unalenga kutoa wigo wa kubadilishana taarifa kuhusu matokeo ya programu na kujadili pamoja kwa umuhimu na kimkakati mafanikio ya LSF kwa miaka ijayo zaidi baada ya mwaka 2021 kwa wanufaika na wadau wote wa LSF. “Hii inakuja kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa LSF wa miaka mitano ijayo unaotarajia kuanza mwakani 2022 mpaka 2026,” alisema na kuongeza kuwa;

“Mkutano huu unalenga kukuza ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa huduma, ushirikishaji wa wananchi katika mifumo ya huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuchochea ukuaji na ustawi wa uwajibikaji, ushiriki na ujumuishwaji wa raia katika mifumo ya uwezeshaji wa kisheria nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Visiwani Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said, akifungua mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 - 21 Oktoba 2021. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala, amesema amefurahi kukutana na wadau wake wote ambao amekuwa akifanya nao kazi nchi nzima, ambapo kwa kipindi cha miaka 10 wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017.

“Nafurahi kukutana na wadau wetu wakubwa ambao mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kutekeleza program yetu ya upatikanaji haki nchi nzima.  Naona fahari kuona kuwa LSF sasa imetimiza miaka 10 tangu ianze kutekeleza program yake na kupitia mashirika wanufaika wake tumefikia mfanikio mbalimbali ya sekta ya msaada wa kisheria.  Naamini kuwa baada ya kikao hiki kazi yetu itaendelea kwa kasi zaidi ili kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kupitia huduma bora za msaada wa kisheria,” amesema Ng’wanakilala.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe amesema anaamini kuwa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa program ya upatikanji wa haki nchini Tanzania litakwenda sambamba na wadau wote wa sekta ya msaada wa kisheria kuelekezana kuhusu kutii matakwa ya kisheria juu ya uendeshaji wa taasisi au mashirika yanatoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Shirika la Legal Services Facility, Ezekiel Joachim, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania bara, Agness Mkawe na Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said wakifuatilia mjadala kutoka kwa wadau wanufaika wa LSF wakati wa mkutano wa siku mbili uliofanyika Jijini Dodoma kwa ajili kufanya tathimini ya utekelezaji wa program ya upatikanaji wa haki nchini Tanzania mwaka 2021.

“Kupitia mkutano huu ningependa kuwakumbusha kuendelea kutii sheria.  Najua waliopo katika mkutano huu ni wakurugenzi ambao ndio watendaji wakuu wa taasisi zenu. Niwaombe kutii sheria zote kama inavyotakiwa.  Kuzingatia sheria zilizowekwa inarahisisha utendaji wenu kwakuwa inasaidia taasisi zenu kutambulika na mamlaka mbalimbali za kiserikali,” amesema Wakili Mkawe.

Baadhi ya Wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria wakifuatilia kwa umakini mada zinazotolewa na wawasilishaji mbalimbali kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF) wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa LSF uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 - 21 Oktoba 2021.

Habari Kubwa