Lubuva atoa neno kwa walioanguka Okt. 25

07Feb 2016
Augusta Njoji
Nipashe Jumapili
Lubuva atoa neno kwa walioanguka Okt. 25

WANASIASA walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana na kuwaingiza madarakani viongozi wa sasa, akiwamo Rais John Magufuli, wametakiwa kuacha kutoa kauli zisizokuwa na tija na badala yake wajipange kwa ajili ya uchaguzi ujao utakaofanyika 2020.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, ndiye aliyetoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano wa tathmini wa asasi za kiraia kuhusu elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Lubuva alisema sasa uchaguzi umekwisha na hivyo wanasiasa waache kuwapotosha wananchi kwani walioshinda tayari wameshinda na walioshindwa wakubali matokeo na kujipanga upya kwa kuandaa sera nzuri zaidi kwa ajili ya uchaguzi ujao. "Kwenye uchaguzi, wananchi ndio wanaohukumu, sio tume… katika uchaguzi mkuu uliopita, Tume ya Uchaguzi haikuwa na chama wala haikupendelea chama chochote, bali ilifanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi," alisema Jaji Lubuva. Jaji Lubuva alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti hili kumkariri aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kuiponda NEC kwa kudai kwamba haina lolote bali inachofanya ni kutumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kukiweka chama hicho tawala madarakani licha ya ukweli kwamba kilishindwa katika uchaguzi mkuu uliopita. Lowassa alikuwa akiungwa mkono na vyama vingine pia vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF). Kwa mujibu wa NEC, Rais Magufuli alishinda kwa kupata asilimia 58.46 ya kura halali huku Lowassa akishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 39.97 ya kura hizo. Akieleza zaidi, Lubuva alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita hakuna hata mgombea mmoja aliyekwenda NEC kuonesha ushahid kuwa aliibiwa kura zake. "Kama ulishinda na kuibiwa kura, ushahidi uko wapi? Mbona hukuuleta? Lakini bado unaongelea kuwa uliibiwa kura… haya ni maneno yasiyo na tija," alisema Jaji Lubuva. Aidha, Lubuva alisema kumekuwapo na maneno kuwa tume inatakiwa ifukuzwe kwa kukipendelea chama fulani, jambo ambalo halina ukweli na wala maneno ya aina hiyo haoni kama yana mashiko. "Tunaendekeza vijimaneno. Vyama vifanye kazi, watu waone na sheria za nchi hazilazimishi watu kujitokeza kupiga kura, lakini elimu ni muhimu ikaendelea kutolewa juu ya ushiriki wa wananchi kwa kujitokeza kupiga kura kwenye chaguzi mbalimbali," alisema Lubuva. Alitolea mfano mwaka 2010 wakati watu milioni 20 walipojitokeza kujiandikisha lakini waliopiga kura walikuwa milioni nane pekee na mwaka 2015, jumla ya watu waliojiandikisha walikuwa milioni 22.5 lakini waliopiga kura ni milioni 15.5. Adha, alisema mwaka 2015 jumla ya asasi za kiraia zilizoomba kutoa elimu ya mpiga kura zilikuwa 551 lakini asasi zilizoruhusiwa kufanya hivyo zilikuwa 447.

Habari Kubwa