Lugola aiagiza Nida kurudisha magari 3 ya vigogo

03Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Lugola aiagiza Nida kurudisha magari 3 ya vigogo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dk. Arnold Kihaule, kuyarudisha magari matatu yaliyokuwa yanatumiwa na waliokuwa vigogo watatu wa mamlaka hiyo.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Akizungumza na viongozi wakuu wa Nida, jana jijini Dodoma, Waziri Lugola alisema magari hayo ni pamoja na lililokuwa la aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Dickson Maimu.

Aliyataja magari hayo kuwa ni linalomilikiwa na Maimu lenye namba za usajili STK 2524, linalomilikiwa na Paul Gwasondi, STK 4671 na STJ 1633, linalomilikiwa na Sabina Nyoni, yote aina Land Cruiser.

Alisema magari hayo yanamilikiwa na watumishi hao kinyume cha taratibu hivyo yanatakiwa kurudishwa Nida.

"Ninakuagiza Mkurugenzi Mkuu hakikisha magari matatu yanayomilikiwa na waliokuwa watumishi wa Nida kinyume cha taratibu yanarudi Nida," alisema.

Aidha, Lugola alimwagiza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa mamlaka hiyo, baada ya vifaa mbalimbali vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 15 ikiwamo jenereta, kompyuta mpakato, kuibiwa kituo cha kuhifadhia kumbukumbu kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani.

Watumishi hao ni Gidson Ivon, Zabron Rusohoka na George Mwandevi.

Juni 18, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wanawashikilia watumishi saba wa Nida kwa tuhuma za wizi vya vifaa vya mamlaka hiyo zenye thamani ya Sh. milioni 15 ambavyo inadaiwa waliviiba na kuviuza.

Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta mpakato mbili, nyaya zake na vitambulisho vya taifa boksi moja lililokutwa na vitambulisho 15,000.

Nyigesa aliwaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa uchunguzi, huiba vifaa hivyo na kuuza ili kujipatia fedha.

Alisema watuhumiwa hao waliiba vifaa wakati ofisi ikihama kutoka ofisi ya awali ya kiwanda chakubangua korosho cha Tanita kilichopo Tumbi, mkoani Pwani kwenda jengo lao jipya la Nida mkoani humo.

"Watumishi hawa waliteuliwa na Nida kuhamisha rasilimali vifaa kutoka ofisi hiyo ya zamani kwenda ofisi mpya za Nida, wakiwa njiani ndipo walipovichepusha na kuviuza kujipatia fedha kwa manufaa binafsi," alisema.

Kamanda alisema taarifa ya tukio hilo zilipokelewa Nida Juni 14 na katika ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi ndipo walipowakamata watumishi hao saba.

"Jumla ya thamani ya mali yote iliyoibiwa ni Sh. milioni 15," alisema.

Habari Kubwa