Lugola amsweka ndani ofisa, amtaka alipe fedha anazodaiwa

10Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
BUNDA
Nipashe
Lugola amsweka ndani ofisa, amtaka alipe fedha anazodaiwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemsweka ndani Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara wilayani Bunda, kwa tuhuma za kutafuna fedha za wanakijiji.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akimuuliza maswali Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, Wilbard Malea, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijji hicho, jana. Mtendaji huyo alikiri kutafuna fedha za wanakijiji hao na aliahidi kuzirudisha.

Waziri Lugola ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo, alitoa amri hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo jana, baada ya kuwataka wenye malalamiko, maswali pamoja na ushauri watoke mbele ili aweze kuwasikiliza.

Zaidi ya wananchi kumi waliojitokeza na kuuliza maswali pamoja na kutoa kero zao, saba kati yao walitoa tuhuma mbalimbali kuhusu Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Wilbard Malea, za kutafuna fedha zikiwamo za maendeleo ya kijiji  na faini anazokusanya kutoka kwa wananchi wanaokwenda kwake kwa ajili ya usuluhishi pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mkazi wa kijiji hicho, Simon Joseph, alimtuhumu mtendaji huyo kuchukua Sh. 91,000 kwenye kikundi chao cha Muungano cha kuweka na kukopa na kudai kijiji kitarudisha fedha hizo, lakini mpaka leo hajazilipa na hakutumwa na serikali ya kijiji kuzikopa.

Pia Happyness Tabonwa, mkazi wa kijiji hicho, alimlalamikia mtendaji huyo kuchukua mbuzi wake watatu baada ya kushindwa kulipa Sh. 50,000, hata baada ya kupata fedha hizo na kumrudishia mtendaji huyo alishindwa kuwarudisha mbuzi hao kwa madai kuwa aliwauza na pesa kazitafuna.

Wananchi hao pia walimlalamikia Waziri Lugola, kuwa wanapopeleka mashtaka kwa mtendaji huyo, watuhumiwa hupigwa faini, lakini fedha ikitolewa haiendi mfuko wa maendeleo ya kijiji bali anazitumia mwenyewe.

Pia mtendaji huyo alilalamikiwa kuchukua simu ya mkononi ya Joseph Japhet, baada ya kuhamia kijijini hapo na kuambiwa alipe Sh. 50,000 kama malipo kwa ajili ya maendeleo kijijini hapo, hata hivyo, fedha hiyo hakuwa nayo ndipo mtendaji huyo alipomnyang’anya simu yake.

Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko hayo, mtendaji huyo alikuwa mbele katika mkutano huo na baada ya kuitwa na Waziri Lugola, ili ajibu tuhuma hizo zikiwamo za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kuwadhulumu wananchi mbalimbali wa kijiji hicho, alikana na baada ya kubanwa huku wananchi hao wakielezea kwa mifano, ndipo alipokiri kutafuna fedha za wananchi hao na kuahidi katika mkutano huo atawalipa wananchi wote wanaomdai.

Baada ya kukiri tuhuma hizo, Waziri Lugola alimwita Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, wilayani Bunda, Mkaguzi Boniface Mwalupale, ili polisi waliopo katika mkutano huo wamkamate na akafunguliwe mashtaka kama atashindwa kuwalipa wananchi wanaomdai.

“Ndugu wananchi, kwanini hawa viongozi mnaowachagua wanakua sio waadilifu? Nimefanya mikutano katika vijiji mbalimbali nimekutana na changamoto kama hii na pia katika kijiji ambacho tumetoka, Mtendaji wa Kijiji pamoja na Mwenyekiti wa kijiji hicho wametafuta fedha za mchanga zilizotolewa na kampuni inayojenga barabara ya Bunda hadi Kisorya, tunaenda wapi ndugu zangu, viongozi wadokozi kama hawa lazima tuwakamate, najua polisi mnahamu ya kukamata mhalifu, mkamateni ili akaeleze hizo fedha alizipeleka wapi na kwanini alizitafuna fedha za wanakijiji,” alisema Lugola.

Akizungumza saa mbili baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara (OCS), Mwalupale alisema mtendaji huyo anadaiwa zaidi ya Sh. 300,000, lakini mpaka sasa ameshatoa Sh. 206,000, hata hivyo hawajamuachia mpaka atakapomaliza kulipa madeni yote.

“Bado hatujamtoa mtuhumiwa huyo ambaye amejipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utapeli, mpaka sasa tayari ametoa 206,000, bado mbuzi watatu hajalipa,” alisema OCS Mwalupale.

Habari Kubwa