Lugola amtwisha mzigo kamishna mkuu Uhamiaji

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Karagwe
Nipashe Jumapili
Lugola amtwisha mzigo kamishna mkuu Uhamiaji

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amempa wiki mbili Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dk. Anna Makakara, kufika katika mikoa ya Kagera na Kigoma kuanza maandalizi ya operesheni kubwa ya kuwaondoa wahamiaji haramu.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola

Amesema operesheni hiyo inatakiwa kufanyika kabla ya uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza Julai, mwaka huu.

Akizungumza na wananchi wa mji wa Karagwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Changarawe mjini hapa, Lugola alisema kuna idadi kubwa ya wahamiaji haramu katika mikoa hiyo, hivyo CGI na maofisa wake wahakikishe wanawaondoa kupitia operesheni kubwa iliyotangazwa.

“Nimepata taarifa za ndani zaidi na pia nyie wananchi hapa mmesema leo (jana) kuhusu uwapo wa wahamiaji haramu, ndiyo maana nimekuja hapa kwa ajili ya kuhakikisha wahamiaji hao wanaondolewa haraka iwezekanavyo hapa Kagera na wa Kigoma,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa licha ya kutangaza operesheni hiyo, aliwataka viongozi wa uhamiaji katika mikoa hiyo kuwa makini mara kwa mara kuhakikisha wanawafuatilia wahamiaji hao kwa kuwashirikisha wananchi waaminifu ili kutoa taarfia sahihi juu ya  wahamiaji hao.

“Tunatarajia kufanya uchaguzi hivi karibuni mwaka huu, hivyo mnapaswa kuhakikisha watakaopiga kura ni Watanzania na si wengineo ili kuepusha usumbufu mkubwa katika jamii,” alisema Lugola.

Lugola aliwataka wananchi wa mikoa hiyo watoe ushirikiano na wasiwafiche wahamiaji hao kwa sababu kumhifadhi ni kosa kisheria, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanatoa taarifa kwa maofisa uhamiaji ili wakamatwe.

Waziri Lugola katika mkutano huo alijibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Karagwe yakiwamo ya wahamiaji haramu ambao pia wanalalamikiwa kuwa wanatumia nguvu ya fedha kuwanyanyasa Watanzania wenye kipato kidogo.

“Pia nina taarifa za kutosha kuwa, baadhi ya maofisa uhamiaji wanapewa fedha na wahamiaji hao ili wasiwakamate. Sasa ole wenu, serikali hii ya Rais (John) Magufuli haichezewi na haijaribiwi. Ole wako wewe ofisa uhamiaji uingie mikononi mwangu, sitakuonea huruma na hakika nitakuondoa kazini,” alisema.

Lugola alisema wahamiaji haramu si wa kuchekewa, hivyo kumtaka CGI ahakikishe anawapanga vizuri maofisa wake kwa kutembea nyumba kwa nyumba kuwasaka na kuhakikisha wote wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

 

 

 

 

Habari Kubwa