Lugola asema hakuna atakayezimiwa simu

14Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Lugola asema hakuna atakayezimiwa simu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewaondoa hofu Watanzania kwa kueleza kuwa hakuna laini ya simu ya mtu itakayofungwa kwa kukosa kitambulisho cha taifa.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, picha mtandao

Kauli hiyo inakinzana na zile zinazotolewa mara kwa mara na maofisa wa sekta ya mawasiliano kuwa laini zote ambazo hazitasajiliwa kwa alama za vidole na kwa kutumia kitambulisho cha mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), zitafungwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Hata baadhi ya watumiaji wa simu ambazo laini hazijasaliwa wakati wa kupiga simu wamekuwa wakihimizwa kusajili kabla ya muda uliowekwa kwa kuwa kushindwa kufanya hivyo, laini zao zitafungwa.

Lugola alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kavuu (CCM), Dk. Pudenciana Kikwembe, ambaye alitaka kupata majibu ya serikali kuhusu wananchi ambao bado hawajapata vitambulisho vya taifa pamoja na kusajili laini za simu.

Alisema lengo la usajili na utambuzi ilikuwa kuwafikia watu milioni 23.3 lakini hadi sasa Watanzania milioni 20.5 wameshasajiliwa, zimezalishwa namba za vitambulisho kwa Watanzania milioni 15.5.

"Naomba niwatoe hofu Watanzania kwamba hakuna mtu yoyote ambaye laini yake ya simu itafungwa kisa hajasajili kwa sababu hana kitambulisho cha taifa," alisema Lugola.

Lugola alisema kazi ya utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao wana sifa za kupata vitambulisho ni endelevu na haina mwisho.

Kwenye mwongozo wake, Kimwembe alisema: "Kwa sasa tunaandikisha vitambulisho vya Nida, Mheshimiwa Mwenyekiti tatizo limekuwa kubwa hasa katika majimbo yetu ya vijijini hususani jimbo langu la Kavuu na Mlele."

"Uandikishaji umekuwa shida na kama tunavyojua mwisho ni Desemba. Naomba kauli ya serikali nini kinafanyika ili kupata vitambulisho?" Alihoji Kikwembe.

Kutokana na mwongozo huo, Lugola alisema: "Naomba niwaondolee wasiwasi Watanzania wote kwamba utambuzi na usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao wana sifa za kupata vitambulisho ni endelevu na haina mwisho wala haina tarehe. Si kweli kwamba ikifika tarehe fulani kama Mtanzania hajapata kitambulisho basi hatapata kitambulisho tena."

"Kwa hiyo Watanzania wasiwe na wasiwasi ni kazi endelevu na ndio maana kila mwaka kuna Watanzania ambao wanafikisha miaka 18. Niwatoe wasiwasi Watanzania wote kwamba maelekezo ya Rais John Magufuli hakuna Mtanzania ambaye simu yake itazuiwa kutumika eti kwa sababu hana kitambulisho cha taifa," alisisitiza.

Lugola alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk. Anord Kihaule na maofisa wake katika wilaya zote kuhakikisha namba ambazo zinatolewa wazipeleke kwa wahusika.

Habari Kubwa