Lugola atoa neno kwa makanisa, misikiti

06Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Lugola atoa neno kwa makanisa, misikiti

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametangaza kuchukulia hatua makanisa na misikiti ambayo haitakwenda kufanyiwa uhakiki.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mwiseni, Kata ya Butimba, Jimbo la Mwibara, Bunda, mkoani Mara, Lugola alisema uhakiki huo unalengo kuangalia taasisi hizo kama zinakwenda sawa kama Sheria ya Usajili inavyoelekeza.

“Serikali iliona ni lazima ifanye uhakiki kwanza kwa lengo la kujua taasisi hizi zinakwenda sawa na sheria za usajili, ndiyo maana hatukuendelea na usajili wa makanisa na misikiti pamoja na taasisi za kiroho,” alisema.

Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara, alitaka taasisi hizo za kidini ziendeshwe kwa mujibu wa sheria na masharti yaliyotolewa na si kujihusisha na mambo ambayo hayahusiki.

Akizungumzia kuhusu vitambulisho vya taifa, Lugola alisema hakuna mwananchi atakakikosa na tayari alishawasiliana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kuwataka watoe namba kwa wakati ili wananchi wafanyiwe usajili wa simu zao za mkononi.