Lukuvi atekeleza agizo la JPM Mkuranga, arejesha Ekari 750

04Aug 2020
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lukuvi atekeleza agizo la JPM Mkuranga, arejesha Ekari 750

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametekeleza agizo la Rais John Magufuli la kurejesha serikalini Ekari 4,222 kwa ajili ya kupimwa na kugaiwa wananchi na nyingine kuendelezwa.

Lukuvi ametekeleza agizo hilo leo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kupokea malalamiko ya wakazi hao wakidai maeneo yao kuvamiwa na wawekezaji.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kazole, Lukuvi ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuchukua Ekari 750 kati ya 1,750 zinazomilikuwa na muwekezaji Soap and Allied Industries, kwa ajili ya kuzipima na kuwagawia wananchi wa eneo hilo bure.

Ameagiza kuwa Ekari nyingine 1,000 zipimwe na kupangiwa kuwekezaji huo ambaye ataeleza aina ya uwekezaji anaofanya na kati ya eneo hilo pia Halmashuari ya itatumia kwa ajili ya huduma za jamii.

"Rais Magufuli ameniagiza kuja hapa, nimefuatilia kwa kina kuhusu mgogoro huu uliodumu kwa zaidi ya miaka 30, haiwezekani mwekezaji akamiliki Ekari 1,750 kwa miaka yote hii lakini ameendeleza asilimia 60 tu, eneo lingine amelitelekeza tena ni la wananchi," amesema Lukuvi.

Ameagiza maeneo hayo kupimwa na Halmashauri kwa ajili ya kuyapima na kuyarasimisha kwa wakazi wa vijiji vyote na maeneo mengine kupangiwa matumizi kwa mujibu wa sheria. 

Sambamba na hilo amesema eneo lingine ni la Ekari 2,472 lilopo eneo la Luzando, wilayani Mkuranga, linalomilikiwa na mwekezaji  ambaye ni  Emtiyaz Ahmed Rajwan na Karim Ahmed Manji.

Amesema sehemu kubwa ya shamba hilo ipo ndani ya vijiji vinne ambavyo tayari vilishapimwa ambavyo ni Luzando, Mwanambaya, Mlaleni na Mipeko.

Amesema wakati wawekezaji hao wakinunua shamba hilo, sehemu kubwa ilikuwa ikimilikiwa na wanakijiji na hivyo tayari wamiliki hao walikuwa wameshatengewa na kumiliki Ekari 1,000 tu kati ya Ekari  2,472 walizomilikishwa wamaliki wa awali.

Lukuvi amesema hati ya shamba hilo pia imewekwa rehani kwa mkopo wa Benki ya CRDB kwa kiwango ambacho hakikutajwa.

"Naagiza eneo hili lirudi kwa Halmashauri kwa ajili ya kulipimwa  na kurasimishwa kwa wananchi wa vijiji hivi vinne na mwekezaji aturejeshee hati yetu na ameshakubali kufanya hivyo," amesisitiza Likuvi.

Habari Kubwa