Lukuvi aagiza fukutwa mashamba pori 21

09Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Kilosa
Nipashe
Lukuvi aagiza fukutwa mashamba pori 21

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameagiza mashamba 24 yaliyoko Kilosa mkoani Morogoro kupelekewa ilani ya kufutwa kutokana na kutoendelezwa.

Lukuvi alitoa agizo hilo jana wilayani hapa alipozungumza na uongozi wa Wilaya ya Kilosa na watendaji wa ardhi katika wilaya hiyo akiwa katika mwendelezo wa ziara ya kutatua migogoro ya ardhi mkoani Morogoro.

Alisema Kilosa haina kumbukumbu za mashamba jambo lililosababisha wizara kuamua kufanya upekekuzi maalum wa mashamba yote katika wilaya hiyo na kubaini mashamba 24 yasiyoendelezwa tofauti na mashamba 48 yaliyopendekezwa kufutwa awali.

Kutokana na agizo hilo, Wilaya ya Kilosa itakuwa na mashamba 72 yanayotakiwa kufutwa baada ya mashamba 48 ya awali kupendekezwa kutokana na kutoendelezwa.

''Maofisa Ardhi wa Wilaya ya Kilosa mfanye upekuzi wa mashama yote yasiyoendelezwa bila upendeleo wala kumwangalia mtu usoni na wala msitishwe na mtu yeyote kwa cheo chake au utajiri wakati wa kufanya kazi hiyo,” alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alisema lengo la serikali kufuta mashamba yasiyoendelezwa ni kuwafikiria wananchi wanyonge wasio na ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na kubainisha kuwa mashamba yatakatayofutwa yatagawiwa kwa wananchi na mengine yatatumika kama ardhi ya akiba itakayotumika kwa uwekezaji.

Aidha, Lukuvi alikemea tabia ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kilosa kuuza au kukodisha mashamba wanayopatiwa na serikali na kusisitiza kuwa katika kukomesha tabia hiyo, wizara inaangalia namna ya kugawa mashamba yaliyofutwa kwa vikundi na kwa wale watakaopatiwa hawataruhusiwa kuuza.

“Mkuu wa Wilaya komesha tabia ya udalali wa mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Kilosa na yale mashamba yanayogawiwa kwa wananchi yatumike kwa shughuli zilizokusudiwa,” alisema Lukuvi.

Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi aliagiza wafugaji wote wanaomiliki maeneo yenye hati kuweka uzio ili kuepuka mifugo yao kwenda maeneo ya wakulima na kusisitiza kufanyika ufugaji wa kisasa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, aliomba kufanyika ukaguzi wa ardhi za vijiji kwa kuwa baadhi yake watu wamejimilikisha, wameuza na mengine kufanyika mgawanyo usio sahihi.

Kwa mujibu wa Mgoyi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeshindwa kufanya uhakiki kutokana na kutokuwa na fedha jambo alilolieleza kuwa limechangia migogoro ya ardhi na kusisitiza kuwa tegemeo la wilaya kwa sasa ni mashamba yaliyofutwa pekee.

Habari Kubwa