Lukuvi atemea cheche  wathamini wa serikali

14Feb 2018
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lukuvi atemea cheche  wathamini wa serikali

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameiagiza bodi ya wasajili wa uthamini wa ardhi kutowasajili maofisa uthamini wa serikali ambao watabainika wamekuwa wakiihujumu kupitia uthamini wa fidia, kodi na mikopo ya benki katika miradi yake.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Lukuvi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi bodi hiyo, ambayo imeteuliwa kwa ajili ya kusimamia kazi hiyo ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikitokea kwa kusababishwa na wathamini wasio waaminifu. 

Lukuvi aliiagiza bodi hiyo kutowapa usajili wa moja kwa hata wathamini wa serikali mpaka pale watakapojiridhisha katika rekodi zao kwamba hawajawahi kushiriki kuihujumu serikali katika uthamini  wa miradi yake mbalimbali ya nyuma.

Alisema hata kama wapo wenye sifa ya kusajiliwa na ambao  wamefanya kazi hiyo kwa muda mrefu, lakini endapo watabainika walishiriki kuiliza serikali katika hujuma hiyo wasipewe usajili na waachwe wakafanye kazi nyingine.

Lukuvi alisema wapo baadhi ya wathamini wa serikali na binafsi ambao wamekuwa wakishirikiana kupanga njama za kujinufaisha wenyewe pale wanapofanya kazi za uthamini kwa kushindwa kutenda haki kwa serikali na wananchi na hivyo kuisababishia hasara kubwa na kuongeza migogoro.  “Kumekuwa na ongezeko kubwa la udanganyifu katika kazi za uthamini hasa katika miradi ya serikali na ya mikopo katika mabenki, kumekuwa na udanganyifu mwingi na tunao uzoefu, wathamini wengi wa private (binafsi) na wa serikali zaidi, wakati wanafanya tathimini ambayo inahusisha kupata kodi serikali mara nyingi wamekuwa wakifanya hujuma ili serikali ipate mapato kidogo, unaweza kujua market value (thamani ya soko) ya jengo fulani ni shilingi kadhaa, lakini linapothaminishwa linapunguzwa kwa sababu hata linapouzwa ukipandisha bei serikali itapata faida,” alisema Lukuvi.

 “Kazi za nje ya serikali zifanywe na watu binafsi na kampuni binafsi ambao watakuwa wamesajiliwa na bodi ambayo imezinduliwa leo(jana).” Alisema kazi ya uthamini imeharibu heshima ya serikali kutokana na wathamini wasio waaminifu ambayo wamekuwa wakifanya udanganyifu na kutanguliza maslahi binafsi.

“Tunayo mifano mingi ambapo serikali imepoteza fedha nyingi sana kutokana na tathmini zilizofanywa na wataalam wetu, kwenye thamani ya nyumba tunapolipa fidia zimekuwa zikiongezwa viwango, lakini kwa kushirikiana na watu wengine wenye nia mbaya,” alisema na kuongeza:

“Napenda kutumia mfano wa mabomu ya Mbagala ambapo katika tathmini ya mwanzo ilionyesha serikali ilitakiwa kulipa Sh. bilioni 12, lakini nilipotaka kujiridhisha  nilibaini ni Sh. bilioni 7 na ilitokea hivyo kwa sababu waliwekwa watu ambao hawakustahili.”

“Na ndio maana ilipotokea ya Gogo la Mboto, tuliona tusitoe thamani ya hela, tuwajengee majengo na hiyo imesababisha  wathamini wamenuna mpaka leo kwa sababu pale chakula hakikupatikana,” alisema zaidi.

 Alifafanua: “Wanaweza wakapandikiza mtu ambaye hana mali, akalipwa pesa zikachukuliwa na  hao wathamini wa serikali, lakini yule mwenye mali halisi akalipwa kidogo, yeyote atakayebainika kupunja thamani halisi ya mtu anayetakiwa kulipwa kulingana na mali yake iliyofanyiwa tathmini achukuliwe hatua, na tunaamini bodi hii itaitendea haki serikali kwa sababu tumeibiwa sana,” alisema Lukuvi.

Pia alipiga marufuku wathamini wa serikali kutofanya kazi binafsi za uthamini ambazo hawajaagizwa na serikali na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali ikiwamo kufukuzwa kabisa.    

Habari Kubwa