Lukuvi awaonya viongozi wa vijiji

27Jan 2017
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Lukuvi awaonya viongozi wa vijiji

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amewaonya viongozi wa vijiji watakaobadilisha kienyeji matumizi ya ardhi bila kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Lukuvi ametolea mfano wa kubadilisha matumizi hayo kama kulisha mifugo kwenye vijiji visivyo na maeneo ya malisho ya mifugo yaliyoainishwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kwenye vijiji vyao.

Aliyasema hayo katika Kijiji cha Kinywang’anga Kata ya Kising’a wilayani humu alipokuwa akikabidhi hati miliki za kimila kwa wanakijiji zaidi ya 800 wa kijiji hicho.

Lukuvi alisema kabla ya kutoa hati miliki za kimila, huanza kwa kutoa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

"Utoaji wa hati kama hizi zitatusaidia sana hasa kiuchumi, kuondoa migogoro, lakini ninasikitika sana kusema baadhi ya vijiji hapa nchini tumefanya kazi kubwa ya kugharimia fedha nyingi, kupanga matumizi bora ya ardhi, tunagharimia kwa kutoa hati kwa fedha nyingi kama hizi, kwa pesa na muda wenu ambao mmetumia, lakini baadhi ya wenyeviti na serikali za vijiji, wanahongwa na kuuza maeneo na kuharibu mpango mzima na akishahongwa, mnakuta ng’ombe wamejaa kwenye kijiji,”alisema Lukuvi na kuongeza:

“Sasa natoa agizo nchi nzima kwa wenyeviti wote nchini, kuanzia sasa tutakapomaliza kupanga matumizi ya ardhi, lazima serikali ya kijiji kwa umoja wenu msimamie matumizi ya ardhi kwa mujibu wa mpango na siyo kazi ya mwenyekiti na serikali ya kijiji itakayoharibu mpango huo lazima niivunje kwa mujibu wa sheria na nitawafukuza wote na nitawashughulikia kwa mujibu wa sheria.”

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinywang’anga, Adam Ngelime, alisema mpango huo utasaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika kijiji hicho na pia kuinua uchumi wa mwanakijiji mmoja mmoja.

Habari Kubwa