Lukuvu amaliza mgogoro sugu wa ardhi Chasimba

22Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Lukuvu amaliza mgogoro sugu wa ardhi Chasimba
  • "Sasa natamka rasmi kuwa ardhi hii imerudishwa kwa wananchi na imeshabadilishwa kutoka kuwa ya biashara na kuwa ya makazi…”

MGOGORO mkubwa wa ardhi katika kijiji cha Chasimba, wilaya ya Kinondoni unaelekea kupata ufumbuzi, baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, kuingilia kati.

Waziri wa Ardhi,Willium Lukuvi

Mgogoro huo baina ya wananchi wa kijiji hicho na mwekezaji wa kiwanda cha Saruji cha Twiga kilichopo Wazo Hill ambao ulianza takribani miaka 15 iliyopita baada ya ya wananchi kudaiwa kuvamia eneo hilo na kujenga makazi.

Ili kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, juzi Lukuvi aliingilia kati kwa kufanya mazungumzo ya amani na muwekezaji wa kiwanda hicho na kumuomba kuwaachia wakazi wa Chasimba sehemu hiyo kwa makubaliano maalumu watakayoafikiana.

Mazungumzo hayo yalizaa matunda kwa muwekezaji huyo kukubali kuachia sehemu ya eneo lake kwa ajili ya makazi ya wananchi hao.

"Sasa natamka rasmi kuwa ardhi hii imerudishwa kwa wananchi na imeshabadilishwa kutoka kuwa ya biashara na kuwa ya makazi, kwa hiyo nimeongozana na wahusika ambao watapanga eneo hili kwa kuzingatia dhana ya mpango shirikishi na kamati ya wananchi itashirikiana na wataalamu wa wizara yetu katika upangaji ili kuwezesha uwekaji wa huduma za kijamii," alisema Lukuvi.

Awali, akizungumza na wananchi hao, Mkurugenzi Msaidizi Usanifu wa Miji na Uendelezaji Upya Maeneo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Immaculata Senje, alisema kuwa eneo hilo lilikjuwa ni mali ya mwekezaji wa kiwanda hicho.

"Ni ukweli eneo hili la Chasimba ni mali ya mwekezaji na ana hati ya mwaka 1957 aliyopewa na wizara yetu inayoonyesha ukubwa na mipaka ya eneo lake, kwa hiyo wananchi ndio walivamia," alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Alfonso Rodriguez, alisema mgogoro huo ulikuwa ni wa mda mrefu na umekuwa ukiwanyima usingizi na kuompongeza Waziri Lukuvi kwa kuumaliza na kuwaahidi wakazi hao kushiriki katika ujenzi wa miundombinu.

Eneo hilo lina takribani kaya 4,096, ikiwa ni wastani wa watu watano kila kaya na jumla ya idadi ya watu ni takribani 20,480.

Habari Kubwa