Lungu kutembelea Tazara

28Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Lungu kutembelea Tazara

Rais Edgar Lungu wa Zambia aliyewasili nchini jana, leo anatarajiwa kutembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na nchi yake, TAZARA, ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo.

Rais Lungu aliwasili nchini jana jioni akiwa ni mkuu wa nchi wa pili kukaribishwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere na mwenyeji wake, Rais Magufuli, baada ya ujio wa Idriss Deby, Rais wa Chad na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais huyo wa Zambia anatarajiwa pia kuzuru shirika la Bomba la Mafuta la TAZAMA, taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ya juzi ilisema.

Baada ya ziara hizo, Rais Lungu na mwenyeji wake watakuwa na mazungumzo Ikulu kabla ya kushuhudia utiaji sahihi wa mikataba minne ya ushirikiano baina ya nchi hizo majirani.

Awali, Deby aliwasili nchini kwa ziara ya siku mbili.

Akiwa nchini, marais Deby na Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watafanya mazungumzo rasmi Ikulu, ambapo watapata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Ukanda wa Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kwa ujumla, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya jana ilisema.

Rais Idriss Deby ni Mwenyekiti wa AU katika kipindi ambacho umoja huo "umeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili bara letu, zikiwemo ugaidi, amani na usalama, na changamoto za maendeleo Barani Afrika," taarifa ilisema zaidi.

Habari Kubwa