Ma-DC, DED wapewa agizo zito wanafunzi wanaozagaa

20Mar 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Ma-DC, DED wapewa agizo zito wanafunzi wanaozagaa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo ameagiza  Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi na Wakuu wa shule nchini, kuhakikisha wanasafirisha wanafunzi waliokosa usafiri badala ya kuwaacha wakizagaa hovyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo.

Machi 17, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifunga shule zote za msingi na sekondari kwa siku 30 kutokana na tishio la ugonjwa wa Corona.

Agizo hilo amelitoa leo Machi 20, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma. 

Amesema baadhi ya mikoa wanafunzi wameonekana kuzagaa na wengine kulala kwenye vituo vya mabasi kutokana na viongozi hao kutotekeleza agizo la kuhakikisha wanasafiri kwa usalama na amani hadi makwao.

"Kama kuna shida wakuu wa shule  wawasiliane na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ambao ni wakuu wa wilaya,  haileti picha nzuri kuona wanafunzi wamezagaa vituoni wakitafuta usafiri jambo ambalo linadhihirisha kuwa wakuu wa shule hawakujipanga vizuri," amesema.

Ametoa pongezi kwa Mkuu wa Shule ya Kilakala iliyopo Morogoro na Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusafirisha wanafunzi hao.

Habari Kubwa