Maabara ya Lancet yaandaa mpango mkakati kujikinga na saratani

10Oct 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Maabara ya Lancet yaandaa mpango mkakati kujikinga na saratani

WATAAM wa Maabara ya Lancet, wameandaa mpango mkakati wa kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga na kubaini ugonjwa saratani ili kuondoka na ongezo la wagonjwa na vifo.

Hayo yalielezwa juzi na Mtaalamu Mkuu wa Maabara kutoka Lancet Dk. Ahmed Kalebi, wakati akikabidhi zawadi na vifaa  tiba kwa  watoto wenye matatizo ya saratani kwenye kituo cha Ujasiri,  kilichopo Hospital ya Taifa ya Muhimbili(MNH) kama sehemu ya kuadhimisha miaka saba ya kutoa huduma za maabara nchini.

Alisema mpango mkakati huo, unatarajiwa kuanza mwakani katika maeneo yote nchini kutoa elimu ya namna ya kutambua dalili, kuwahi kupata matibabu ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaopoteza maisha kutoka na kuchelewa kupata matibabu.

“Kama Lancet, tunakamilisha mpango kazi wa kufanya kmapeni ya kuongeza uelewa kwa jamii  nchi nzima ili jamii itambue ugonjwa huu, kupitia dalili zake  na kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara,” Dk. Kalebi alisema.

Dk Kalebi alisema wamekuwa na utaratibu wa kusaidia watoto waliothirika na ugonjwa wa satarani kila mwaka kama sehemu ya majukumu yake.

Kuhusu msaada huo, alisema zawadi zilizokabidhiwa ni dawa na vifaa tiba, vifaa vya kupima joto na shinikizo la damu,vitabu na vifaa vya shule.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano MNH, John Steven, akipokea msaada huo, alisema hospital hiyo imekuwa ikipokea watoto wenye ugonjwa wa saratani  kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Alisema MNH pia imechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwapatia huduma bora  kwa wagonjwa wa Saratani ikiwamo tiba ya mionzi na kuwaruhusu kurudi nyumbani pale afya zao zinapokuwa zimeimarika.

“Naiomba jamii nzima kujitolea kuwasaidia watoto wenye maradhi ya saratani kama sehemu ya upendo wao wa binadamu. Pia naomba jamii kujenga utaratibu wa kupima mara kwa mara ili kuubaini ugonjwa, kwa sababu ukiuwahi unapona,”Steven alisema.

Naye Mama Mlezi wa kituo hicho. Hawa Mpina, alisema wanapokea watoto wenye saratani kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuishi nao wakati wakiendelea na matibabu.

Alisema kituo hicho pia kimewahi kuwatibia watoto kutoka nchi za jirani kama Burundi na Nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao hulazimika kuishi kituoni hapo.

Habari Kubwa