Maabara zafanywa madarasa

16Jan 2017
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Maabara zafanywa madarasa

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imebadili matumizi ya vyumba vya maabara katika shule tatu za sekondari kwa kuvifanya madarasa.

Mabadiliko hayo, imeelezwa, ni mkakati wa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madarasa kwa wanafunzi zaidi ya 200 wa kidato cha kwanza ambao wanakabiliwa na hatari ya kuchelewa kuanza masomo.

Ofisa Elimu Sekondari mkoani humu, Lidia Helbert, jana alizitaja shule ambazo vyumba hivyo vya maabara vimebadilishwa matumizi kuwa ni Sinde, Mwakibete na Uyole.

Alisema kwamba awali wanafunzi 352 wa kidato cha kwanza katika jiji hili walikuwa katika hatari ya kuchelewa kuanza masomo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, lakini idadi hiyo ilipungua na kufikia 214 baada ya shule tatu kukamilisha ujenzi wa madarasa mapya.

Helbert alizitaja shule za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa madarasa kuwa ni Mponje, Itezi na Uyole ambazo zimechukua wanafunzi 138.

“Baada ya agizo la Mkuu wa Mkoa (Amos Makalla) la kutaka wanafunzi wote wa kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati, sisi tumeamua vyumba vya maabara ambavyo bado vifaa havijapatikana, vitumike kwa muda kama madarasa ili kutimiza agizo hilo," alisema.

"Shule ambazo vifaa na kemikali zipo tumeamua vifaa hivyo viondolewe na kuhifadhiwa kwenye vyumba vya maandalizi ili wanafunzi wasije wakadhurika."

Alifafanua kuwa vyumba hivyo vitatumika kwa muda wa wiki mbili pekee kwa matarajio kuwa vyumba vya madarasa vinavyojengwa vitakuwa vimekamilika.

Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, alisema halmashauri yake ilichangia Sh. milioni mbili katika kila shule iliyokuwa na upungufu wa madarasa ili kusaidia juhudi za wananchi kufanikisha ujenzi huo.

Alisema lengo lilikuwa kuhakikisha hadi wakati shule zinafunguliwa Jumatatu iliyopita, vyumba vyote vilivyokuwa vinajengwa viwe vilishakamilika na wanafunzi kuanza masomo, lakini wakashindwa kufikia na kuamua vyumba vya maabara vitumike kama madarasa kwa muda.

Meya Mwashilindi alisema lengo ni kuona wanafunzi wote wa kidato cha kwanza wanaanza masomo kwa wakati mmoja ili wasitofautiane katika kuendana na mtaala.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Makalla, ameipongeza halmashauri, Bodi za Shule na wananchi kwa hatua waliyoifikia katika kukamilisha vyumba vya madarasa na uamuzi wao wa kutumia kwa muda vyumba vya maabara kama madarasa.

Alisema zoezi hilo la kubadili matumizi ya maabara haitaathiri masomo yanayotegemea maabara hizo kwa kuwa ndani ya siku 14 vyumba vya madarasa vitakuwa vimekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutumika.

Habari Kubwa