Maafisa afya Katavi watakiwa kusimamia usafi

18Jan 2022
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Maafisa afya Katavi watakiwa kusimamia usafi

MAAFISA afya wa mkoa wa Katavi, wametakiwa kuzingatia ukaguzi wa usafi wa mazingira katika maeneo muhimu ya biashara ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza leo Januari18, 2022 katika kikao cha maafisa hao kilichofanyika ukumbi wa idara ya maji katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Katibu Tawala wa Mkoa, Rodrick Mpogolo, amesema eneo la biashara ya nyama linalotakiwa kuangaliwa kwa ukaribu kwenye swala la usafi.

Mpogolo amesema walifanyie kazi suala la usafi wa nyama kuanzia kwenye machinjio na usafiri unaotumika kusafirisha nyama hiyo kuelekea buchani.

"Tunalo jukumu la kufanya, maana yapo maeneo ni lazima tuyafikie ili tuweze kuboresha suala la usafi lazima tuwapange wafanya biashara, bodaboda, natamani kuona nyama zinauzwa mazingira salama kuna nyama zinasafirishwa kwenye baiskeli hii siyo sawa na sio nyama tu hata mikate," amesema Mpogolo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Katavi Dk. Omar Sukari, amesema kwa kuhakikisha wanasimamia suala zima la usafi na afya za watu watakaa kikao kwa kushirikisha sekta mbalimbali ikiwemo maji, barabara, elimu, wakurugenzi, wakuu wa wailaya pamoja na makundi ya wafanya biashara.

"Lengo la kikao tutakachokifanya ni kuhakikisha tunaepuka hili gonjwa la kipindupindu na magonjwa mengine ya milipuko maana kupitia kikao hicho kila mtu atajua akasimamie eneo gani, pia tutafatilia sehemu uliotuelekeza hasa kwenye uchakataji wa swala la nyama," amesema Dk. Sukari.

Kwa mujibu wa afisa afya wa mkoa Suzane Komba, amesema kikao hicho cha maafisa afya ni kwaajili ya kuweka mikakati ya kuhakikisha mkoa unakuwa na vyoo bora katika halmashauri zote.

Amesema wanataka kusiwepo na kaya isiyokuwa na choo bora ikiwemo pia watajitahidi kusimamia miundo mbinu ya choo katika vituo mbalimbali vya afya.

"Kila kaya kuwe na vyombo vya kunawia mikono na maji tililika na sabuni hiyo ndio njia bora ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu, na kuharisha wanasema nyumba ni choo maisha ni kubalansi lakini nyumba ni choo," amesema.

Baadhi ya maafisa afya walioshiriki kikao hicho, akiwemo Erick Kisaka, kutoka manispaa ya Mpanda, Dulla Makala (Nsimbo), Ridhiwan Mohamed, (Mpimbwe) na Henrick Mwasibale (Tanganyika), wamesema watayafanyiakazi maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kusimamia usafi kila eneo na kuwa na vyoo bora kwa kila kaya.

Habari Kubwa