Maagizo ya JPM lawatesa vigogo Wizara ya Madini

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Maagizo ya JPM lawatesa vigogo Wizara ya Madini

AGIZO la Rais John Magufuli kuhusu Wizara ya Madini limeonekana kuwatesa viongozi wakuu wa wizara hiyo baada ya kukutana na kutafakari namna ya kulitekeleza.

Waziri wa Madini, Doto Biteko, picha mtandao

Katika kufanya hivyo, Waziri wa Madini, Doto Biteko, juzi alikutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini, Taasisi zake pamoja na Wenyeviti wa Tume ya Madini na Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico), jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, Biteko na viongozi hao walijadili namna ya kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli aliyoyatoa wakati akimwapisha Waziri Biteko kushika wadhifa huo Januari 9, mwaka huu.

Biteko aliwataka watumishi  wa wizara na taasisi zake ambao hawayajayasikiliza maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli kuhakikisha kuwa wanayasikiliza ili kuweka uelewa wa pamoja na kushirikiana katika kutekeleza majukumu  ya wizara kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya madini inaimarika.

 “ Tuliulizwa dhahabu inauzwa wapi? Basi tusisubiri tena Rais atuulize inauzwa wapi,” alisisitiza Biteko.

Pia alisisitiza kuwapo kwa ushirikiano miongoni mwa watumishi wa wizara katika utekelezaji wa majukumu hayo na kusisitiza kuhusu mabadiliko yanayoonekana kupitia sekta ya madini ikiwemo kufanya kazi na kuongeza kuwa: “Kinachotuunganisha mahali hapa ni kazi na wala si dini au jambo lingine.”

“Kiu kubwa ya Rais ni kuona Watanzania wote wananufaika na rasilimali madini na kuona taswira nzuri inajengeka kuhusu sekta ya madini ikiwamo kufanya kazi kwa weledi.

“Vipaji mlivyo navyo mvitumie vizuri vitoe matokeo yanayoonekana. Fanyeni kazi ambazo zitaacha matokeo yatakayodumu. Natamani ningezungumza na watumishi wote ili kila mmoja aelewe kile ninachosema,” alisema.

Biteko pia aliwataka watendaji kuchukua hatua badala ya kutumia muda mrefu kutafuta miongozo wanapotekeleza majukumu yao jambo ambalo linachelewesha utekelezaji wa majukumu.

“Unasubiri mwongozo gani ilhali unayo Sheria ya Madini? Alihoji.

Biteko alitumia nafasi hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, na kumwelezea kuwa ni kiongozi ambaye amemfundisha mambo mengi.

“ Namshukuru sana dada yangu, rafiki yangu Angellah. Alinipokea vizuri sana. Hakuna ushirikiano nilioukosa kwake. Amenifundisha mengi ikiwamo kukaa kwenye kikao na kujadili mambo kwa kina,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alilitaka Shirika la Madini (Stamico) kuanza kutoa gawio kwa serikali na ikiwezekana, jambo hilo lifanyike kabla ya mwaka ujao wa fedha.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali (mstaafu) Michael Isamuhyo, alimweleza Waziri Biteko kuwa anayapokea majukumu yote yaliyo mbele yake kuhakikisha shirika linatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Habari Kubwa