Maajabu 10 ya tende na maziwa kwa wanandoa

03Sep 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Maajabu 10 ya tende na maziwa kwa wanandoa

AMA kweli mchanganyiko wa tende na maziwa una maajabu yake. Kwa mujibu wa wataalamu, mchanganyiko mzuri wa vyakula hivyo huweza kumnufaisha mlaji kwa mambo 10 muhimu ya kiafya, mojawapo ikiwa ni kuwaongezea wanandoa nguvu na hamasa ya kushiriki harakati za kujenga familia yao kwa furaha zaidi.

Ripoti za tafiti mbalimbali za masuala ya lishe zinathibitisha juu ya maajabu hayo ya mchanganyiko tende na maziwa, huku mmoja wa wataalamu akikiri kwamba vyakula hivyo vinapoliwa kwa pamoja, huwa ni sawa na ‘dozi’ matata yenye kuwaongezea makali ya kuridhiana kinyumba baina ya wanandoa.

Aidha, tende na maziwa huwa na uwezo pia wa kuwaondolea walaji uwezekano wa kupata maradhi mbalimbali yakiwamo ya saratani na chanzo cha kuwa na uwezo huo ni wingi wa virutubisho vinavyopatikana ndani ya mchanganyiko wa vyakula hivyo.

UNDANI WA MAAJABU 10
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, mtaalamu wa masuala ya lishe aitwaye Jolenta Joseph, alisema kuwa kwa pamoja, baadhi ya virutubisho muhimu vinavyopatikana ndani ya mchanganyiko wa vyakula hivyo ni pamoja na vitamini B1, B2, B3, B5,  A1 na C.

Vingine ni Calories (nishati) na madini yakiwamo ya Calcium, Potassium, Magnesium, Phosphorous, kiinilishe cha Folate na pia wanga.

Joseph alitaja mambo 10 ya faida yanayoweza kupatikana kwa ulaji wa mchanganyiko kama juisi ya tende na maziwa kuwa ni pamoja na kuwaongezea nguvu na ubora wa mbegu wanaume walio na tatizo hilo; pili ni kuinua hamu na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kwa kina mama; tatu kuimarisha afya ya mama mjamzito na kichanga chake; nne ni uwezo wa kusaidia kuondoa vilevi mwilini (hasa kwa wanywaji pombe); tano ni uwezo wa kuukinga mwili dhidi ya magonjwa kama saratani ya tumbo na kiharusi; sita ni kusaidia mchakato wa usagaji wa chakula tumboni; saba ni faida ya mchanganyiko huo kuondoa tatizo la ukosefu wa choo au mtu kupata choo kigumu; jambo la nane ni uwezo wa kumuondolea mtu uchovu; tisa ni kuongeza damu mwilini kutokana na kujaaliwa wingi wa madini chuma na kumi, ni uwezo wa kusaidia mishipa ya fahamu kufanya kazi yake vizuri.

Akifafanua kuhusu faida hizo, Joseph alisema Wanasayansi mbalimbali duniani wamebaini uwezo wa mchanganyiko wa tende na maziwa katika kuupa mwili lishe muhimu na hivyo akashauri kuwa ni vyema kila mmoja kula vyakula hivyo kwa ajili ya kuimarisha afya yake, bila kujali jinsia.

Jolenta alisema tende ina protini na hivyo, faida hiyo huwa maradufu zinapoliwa kwa kuchanganywa na maziwa ambayo pia yana protini kwa wingi.

Alisema tende zina kiasi kidogo cha mafuta yasiyo na rehemu na protini yake inapokuwa na maziwa huwasaidia watu wote, yaani wanawake na wanaume, hasa katika masuala ya afya ya uzazi.

Joseph alisema mchanganyiko wa vyakula hivyo huwasaidia wajawazito kwa sababu huwa na madini ya chuma kwa wingi na mjamzito anapotumia humfanya kuwa na kiasi cha damu cha kutosha na mwishowe kuzaa salama na kuwa mwenye afya njema.

“Mchanganyiko huu humrahisishia mjamzito kuzaa salama kwa sababu tende ina sukari ambayo huwapa nguvu wajawazito katika kusukuma mtoto wakati wa kujifungua… bila nguvu uzazi huwa mgumu,” alisema.

Alisema tende husaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa choo au mtu kupata choo kigumu kwa sababu tunda hilo limejaaliwa kuwa na nyuzi nyuzi (fibers) ambazo husaidia uyeyushaji wa chakula na hilo hufanyika vizuri kwa kula na maziwa.

“Pia huondoa uchovu mwilini kwa sababu ina virutubisho vya sukari asilia kama glucose, sucrose na fructose,” alisema Joseph.

Aidha, alisema madini ya potassium yaliyomo ndani yake husaidia kumwepusha mtu na maradhi ya kiharusi na ina kiasi kidogo cha chumvi ambayo husaidia kuimarisha mishipa ya fahamu.

“Tende husaidia kupunguza lehemu mwilini na kwa wale wenye matatizo ya ugonjwa wa kukauka damu mwilini tende inaweza kuwapa ahueni kubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Tende ina vitamin A ambayo husaidia uoni mzuri na kuukinga  mwili na maradhi, pia ina madini ya chuma ambayo kazi yake ni kuzalisha chembechembe nyekundu za damu na ndiyo maana zinapoliwa na maziwa huwa na msaada mkubwa kwa wajawazito.

MAANDALIZI
Kwa mujibu wa Joseph, mchanganyiko wa tende na maziwa huweza kuandaliwa kwa namna nyingi na mojawapo ni kuchukua tende zilizoiva kiasi cha kujaa kiganja kimoja cha mkono, kuondoa kokwa zake kisha kuchanganya na glasi ya maziwa mabichi (fresh) kulingana na mahitaji.

Baada ya hapo, mchangayiko huo usagwe kwa pamoja ili kupata rojorojo kama juisi nzito inayoweza kunywewa au kuwekwa kwanza kwenye friji ili ipate baridi kabla ya kutumiwa.

Habari Kubwa