Maajabu 20 ya Bamia kwa afya

08Oct 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Maajabu 20 ya Bamia kwa afya

LICHA ya bamia kuchukuliwa na wengi kuwa ni chakula rahisi kinachotumiwa zaidi na kundi la watu wa uchumi wa chini na kati, ukweli kwamba aina hiyo ya mboga ina maajabu ya aina yake mwilini.

Kwa mujibu wa wataalamu, walaji wa bamia hunufaika kwa kupata utitiri wa viinilishe vilivyomo kwenye zao hilo, ambavyo mwisho wa siku humpatia mlaji faida za kiafya takribani 20, ikiwamo ya kuongeza utimamu wa moyo.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Daktari katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mshamu Abdallah Mwindah, alisema mojawapo ya faida za ulaji wa bamia ni kuwasaidia wanawake kuepukana na changamoto za kiafya zinazojitokeza kwa baadhi yao ambao huwa na siku zisizotabirika za mizunguko yao ya kila mwezi.

“Wapo wanawake wanaosumbuliwa na hedhi za mara kwa mara. Ulaji wa bamia utawasaidia kuondokana na tatizo hili,” alisema Dk. Mwindah.

Dk. Mwindah aliongeza kuwa virutubisho vilivyomo ndani ya bamia husaidia kukabili magonjwa mbalimbali yatokanayo na kujamiiana ikiwamo kaswende na kisonono.

Aidha, alitaja faida nyingine za ulaji wa bamia kuwa ni kuondoa vimelea vya sumu kwenye ngozi ya mwanadamu.

“Bamia husaidia pia kukabili ugonjwa wa pumu. Huongeza kinga ya mwili na mtu akiwa na kinga ya mwili, hawezi kushambuliwa na maradhi mara kwa mara,” alisema.

Daktari huyo alitaja faida nyingine ya ulaji wa bamia kuwa ni kupata virutubisho aina ya nyuzinyuzi ambavyo husaidia katika kusaga chakula mwilini.

Kadhalika, faida nyingine iliyopo kwenye bamia ni protini ambazo husaidia kujenga mwili.

Dk. Mwindah alisema ulaji wa bamia husaidia pia kuimarisha afya ya nywele, kupambana na tatizo la uchovu wa mwili na pia msongo wa mawazo.

“Kwa wale wenye tatizo la choo, ulaji wa bamia husaidia kuondokana na tatizo hilo. Bamia husaidia vilevile katika kurekebisha kiwango cha sukari mwilini,” alisema.

Mtaalamu huyo alitaja faida nyingine ya ulaji wa bamia kuwa ni kuusaidia mwili kusafisha damu.

“Ulaji wa bamia husaidia kutibu tatizo la upungufu wa damu. Husaidia pia kumtibu mtu mwenye matatizo ya vidonda vya tumbo, huondoa sumu mwilini na faida nyingine ni kuimarisha mifupa pamoja na mfumo wa uonaji kwa sababu ina chanzo kizuri cha vitamini A na Beta Carotene, ” alisema Dk. Mwindah.

Aidha, katika baadhi ya majarida ya lishe, inaonekana kuwa bamia husaidia mwili pia kukabiliana na baadhi ya saratani.

“Mapishi ya bamia yapo ya aina nyingi, mojawapo ni kuchemsha kabla ya kula na hata kuyakausha kwa jotoridi la wastani…yapo maandalizi mengi na ulaji wake una faida nyingi mwilini,” ilielezwa na mmoja wa wataalamu wa masuala ya lishe.